EWURA CCC SHINYANGA YARIDHISHWA NA MIRADI YA MAJI INAYOTEKELEZWA NA SHUWASA TINDE NA DIDIA

Wajumbe wa EWURA  CCC mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye Tangi la Mradi wa Maji Ziwa Victoria lililopo kijiji cha Buchama Tinde Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Kamati ya Watumiaji wa Huduma za Maji na Nishati zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA Consumer Consultative Council - EWURA CCC) Mkoa wa Shinyanga imefanya ziara kutembelea Miradi miwili inayotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) iliyopo kata ya Tinde halmashauri ya Shinyanga Mkoani humo.

Akitoa ufafanuzi wa gharama za miradi na wanufaika wa miradi hiyo, wakati wa ziara hiyo iliyofanyika leo Agosti 17,2023, Kaimu Mkurugenzi Usambazaji Maji na Usimamizi wa Usafi kutoka SHUWASA Mhandisi Uswege Mussa amesema Mradi wa maji Didia umegharimu Shilingi Milioni 92 wenye Ujazo wa lita 94,000 wanaotarajia kunufaika ni wakazi 9,210 na Mradi wa maji Tinde Tanki la Buchama lenye ujazo wa lita Milioni 1,150,000. utawanufaisha wakazi 60,000 lakini kwa hatua za awali mpaka sasa wananchi 10,129 wa vijiji viwili kijiji cha Jomu na Nyambui wameanza kunufaika na Mradi huo.
Kaimu Mkurugenzi usambazaji maji na usimamizi wa usafi kutoka SHUWASA Mhandisi Uswege Mussa akitoa ufafanuzi wa gharama za miradi na wanufaika wa miradi hiyo.

Mwenyekiti wa EWURA CCC Mkoa wa Shinyanga, Kudely Sokoine amesema Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo inayotekelezwa na Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA).

''Niwapongeze sana SHUWASA kwa utekelezaji wa miradii hii kwa sababu maji ni Uhai bora mtu alale gizani kuliko kukosa maji kupitia ziara hii tumeona fedha za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan zinaonekana sisi kama kamati tutaenda kuwa Mabalozi wazuri kwa wananchi kwa sababu tunaweza kuwa tunawalaumu SHUWASA kumbe sisi watumia maji ndiyo hatulipi kwa wakati tukichelewa kulipa tunawapatia shida hawa Mamlaka kwa sababu na wao wananunua kutoka kwa KASHWASA", amesema Kudely.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kudely Sokoine akizungumza wakati wa ziara hiyo.

Naye Mweka Hazina wa Kamati ya ushauri wa watumia maji na nishati Mkoa wa Shinyanga Joseph Ndatala ameiomba SHUWASA  kusambaza maji haraka kwa wananchi kwani huduma bora ni haki ya kila mwananchi.


"Miongoni mwa huduma za msingi na lazima kwa binadamu yeyote ni Maji, miradi hii isikamilike tu halafu wananchi wasinufaike na miradi hii tuhakikishe wananchhi wanapata huduma ya maji kwa sababu huduma bora ya maji ni haki ya kila mwananchi wa Tanzania'', amesema Ndatala.
Mweka hazina wa Kamati ya ushauri wa watumia maji na nishati mkoa wa Shinyanga Joseph Ndatala akizungumza wakati wa ziara hiyo.

Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Tinde Edward Charles na Mlila Tumaini Bwile wameshukuru kuwepo kwa huduma hiyo kwani hapo awali walikuwa wananunua dumu moja la maji Tshs 500/= mpaka 1000/= nyakati za kiangazi huku wakiiomba Mamlaka husika kuangalia bei ambapo kwa Unit moja wananunua kwa Tshs 2,500/= hali inayowapa ugumu wananchi wa kipato cha chini kupata huduma ya maji safi na salama.

Akifafanua kuhusu bei hiyo Mkurugenzi Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira  Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola amekiri uwepo wa bei kubwa ya maji kwenye maeneo hayo huku akiwaomba wakazi wa maeneo hayo kuwa watulifu wakati jambo hilo linashughulikiwa.

"Ni kweli kwa maeneo haya ya Tinde kuna bei kubwa ya kununnua maji jambo hili tunalifanyia kazi kufika mwezi wa 9 au wa 10 bei zitakuwa zimeshuka", amesema Katopola.
Mkurugezi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mkoani Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza kwenye mradi wa Tangi la maji Tinde.
Mradi wa Tangi la maji Didia.

Mkazi wa kata ya Tinde Edward Charles.
Mkazi wa kata ya Tinde Mlila Tumaini Bwile.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post