Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KITUO CHA TGC CHAMKABIDHI KATIBU MKUU MAHIMBALI TUZO YA KUTHAMINI MCHANGO WAKE UONGEZAJI THAMANI MADINI

 


Na Mwandishi wetu -Dodoma 

Watumishi wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) wamemkabidhi tuzo maalum ya shukrani Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini.


Akikabidhi tuzo hiyo kwa Katibu Mkuu katika Hafla hiyo fupi iliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara ya Madini, Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma Agosti 21, 2023, Mratibu wa TGC, Daniel Kidesheni amesema kuwa tuzo hiyo iliyotengenezwa kwa kutumia madini ya vito mbalimbali ina muundo wa pembe tano (pentagon) unaowakilisha taasisi tano zilizopo chini ya Wizara ya Madini.




Taasisi hizo ni Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na pamoja na Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI).


Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Katibu Mkuu Kheri Mahimbali amewashukuru watumishi wa TGC kwa kuthamini mchango wake katika kuimarisha shughuli za uongezaji thamani Madini nchini na kuahidi kuendelea kuwapa ushirikiano katika kutimiza malengo ya kituo hicho.


Kituo cha TGC ni Kituo kinachotoa mafunzo ya uongezaji thamani madini, kinachomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kinafanya kazi chini ya Wizara ya Madini.


Malengo ya TGC ni kudumisha ubora, viwango, uadilifu na taaluma katika utoaji wa huduma zinazohusiana na madini ya vito ili kufikia viwango vya kimataifa vinavyotakiwa katika soko la kimataifa.
Kituo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo yanayolenga kuzalisha wataalam wenye ujuzi katika shughuli za uongezaji thamani katika Madini hususani utengenezaji, ukataji, na ung'arishaji wa Madini ya Vito.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com