KITUO MAHIRI CHA USIMAMIZI WA MAZAO YA NAFAKA KONGWA MWAROBAINI WA SUMUKUVU




Na Dotto Kwilasa, DODOMA

Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha na kuinua uzalishaji katika kilimo na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa unaotokana na Sumukuvu .

Kituo hicho kitatumika kuiimarisha tafiti za kilimo na ubunifu na kutoa majawabu kwa changamoto zinazojitokeza katika kilimo, kama vile mabadiliko ya tabianchi.

Ili kufanikisha hilo tayari imeshatekeleza ujenzi wa Kituo Mahiri cha Usimamizi wa Mazao ya nafaka ambacho kitatumika kudhibiti sumu kuvu kilichopo eneo la Mtanana Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Akiweka jiwe la msingi kwenye kituo hicho,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amesema anasema ujenzi wa kituo hicho ni suluhisho la changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wakulima pindi mazao yao yanapozuiliwa katika masoko kutokana na tatizo la sumu kuvu.

Ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kutoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo katika kupambana na sukumuvu mkoani Dodoma ambapo jumla ya Wakulima 12,517 wamepatiwa mafunzo kupitia mradi huo na kuitaka Wizara kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima.

Makamu wa Rais ameielekeza Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Mbegu (ASA) kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora na zenye bei nafuu kwa wakulima pamoja na kufanya udhibiti wa mbegu feki kwa kukagua wauzaji na wazalishaji wa mbegu hizo.

"Nawaagiza watendaji wa Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Umwagiliaji kufanyia kazi ombi la wananchi wa Mtanana kuhusu bwawa la umwagiliaji litakalosaidia kuondoa adha ya mafuriko ya mara kwa mara katika eneo hilo pamoja na kukuza kilimo kwa njia ya umwagiliaji, "amesema

Halikadhalika Dk. Mpango ametoa wito kwa Taasisi za utafiti ikiwemo TARI kuangazia mazao mapya yanayoweza kustawi mkoani Dodoma kwa kuwa ardhi hiyo ina fursa ya kuzalisha mazao mengi.

"Viongozi wote mkiwemo Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya punguzeni muda wa kukaa ofisini na badala yake watembeleeni wananchi kutatua changamoto zinazowakabili, " amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema mradi wa kituo Mahiri cha Usimamizi wa Nafaka unahusisha kiwanda cha kuchakata unga ambapo Wizara imedhamiria kuongeza mitambo ya kuchanganya virutubisho na kuepusha changamoto zinazojitokeza za hitajio la kuchanganya virutubisho nje ya nchi.

Bashe ameongeza kwamba Kiwanda kilichopo katika kituo hicho kitaruhusu wakulima wadogo kutumia kuchakata mahindi yao kwa gharama nafuu zaidi na kuwauzia wateja wao.

Amesema Kituo hicho kitachangia katika kujenga mtandao wa wakulima, taasisi za serikali, na wadau wengine, hivyo kuimarisha ushirikiano na mshikamano katika jamii ya wakulima.

"Wizara itatengeneza utaratibu mpya wa usimamizi wa mbegu za mahindi ili kuondoa mbegu feki,aidha Wizara haitasita kufuta leseni za wazalishaji wa mbegu ikiwa mawakala wao watatumia majina ya mbegu hizo kuuza mbegu feki sokoni, " Bashe amesema

Bashe amesema pamoja na faida nyingine lukuki za kituo hicho pia kitatoa mafunzo ya maarifa na mbinu zinazoweza kusaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kama ukame na mafuriko kwa maendeleo endelevu kwa jamii.

Amesema, "Tutahakikisha Mazingira ya soko la mazao yote linakuwa lenye uhalisia kwa kuhakikisha mauzo yanafanyika kwa kutumia vipimo halali badala ya kukadiria na kwamba mazao yote hayakumbwi na sumu kuvu, " anasisitiza Bashe

Naye Mbunge wa Kongwa Job Ndugai ameeleza faida zitakazopatikana kutokana na uwepo wa kituo hicho kuwa kitasaidia wananchi wengi kuwekeza kwenye kilimo na kuondokana na hofu ya sumu kuvu iliyokuwa imewatawala

Amesema uzalishaji wa chakula utaongezeka mara dufu hivyo kusaidia kupunguza njaa na kuhakikisha usalama wa chakula hali itakayosaidia kuboresha lishe na afya ya wananchi.

Ndugai ameongeza kuwa kituo hicho kitaimarisha Uchumi wa Vijiji na Mitaa kwa kuwa kilimo kitachochea maendeleo ya kiuchumi kupitia wakulima kuwa na fursa za masoko na hivyo kuongeza mapato yao, ambayo yanaweza kutumika kuboresha maisha yao na familia zao.

"Sekta ya kilimo inatoa nafasi nyingi za ajira, kutoka kwa wakulima hadi wafanyakazi wa usindikaji,nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wa Kongwa kuwekeza kwenye kilimo kutasaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuwa na maisha mazuri, " amesisitiza

Nao baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kongwa wameipongeza hatua hiyo ya serikali kujenga kituo mahiri cha kudhibiti sumukuvu kuwa kitasaidia kuokoa maisha ya watu baada ya kutumia mahindi yenye viambata vya sumukuvu huku wengine wakipoteza maisha kwa Kansa ya ini .

"Sasa tuna uhakika wa kulima kwa kujiamini na hatuogopi tena sumukuvu, tu naomba Serikali sasa itusaidie kuondokana na ukosefu wa mbegu bora,tunalima lakini tunapata mazao hafifu kunasababisha umaskini,tunaomba pia kuhusu masoko ya mifugo serikali iingilie kati kuwaondoa madalali wa mifugo, "amesema mmoja wa wakulima Margaret Mazengo.

Pamoja na mambo mengine katika muktadha wa maendeleo ya kilimo, Kituo hicho Mahiri cha Usimamizi wa Mazao kilichopo Kata ya Mtanana kinatoa nafasi ya pekee katika kuboresha uzalishaji na maisha ya wakulima.

Kituo hiki kina lengo la kushughulikia changamoto zinazowakabili wakulima, ikiwa ni pamoja na kushughulikia kero zote zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, upatikanaji wa taarifa sahihi, na usimamizi wa rasilimali.

Chipanha Kusenha anasema ili wananchi wanufaike na mradi huo wa kimkakati ni lazima Mafunzo ya Kilimo Bora yatole kwa wakulima Mara kwa Mara na hii itasiaida kuondokana na tatizo la sumukuvu ambayo imekuwa ni tatizo la muda mrefu kwa wakulima wengi hii itasaidia kuboresha mavuno pamoja na matumizi sahihi ya mbolea, mbegu bora, na teknolojia za kisasa.

"Mradi huu ni wa kimkakati ambao serikali imetoa fedha nyingi hivyo Sisi wakulima lazima tuendane na kasi ya telnolojia za kisasa kuhusu utoa elimu juu ya matumizi bora ya maji na udongo,kilimo cha umwagiliajo,kusaidia wakulima kupunguza gharama na kuimarisha uzalishaji na watafiti kutoa ushauri wa kitaaluma kuhusu magonjwa ya mimea na wadudu, na jinsi ya kuyadhibiti kwa ufanisi, "anasema Kusenha.

Kituo Mahiri cha Usimamizi wa Mazao ni chombo muhimu katika kuboresha kilimo na maisha ya wakulima katika Kata ya Mtanana na Dodoma kwa unumla kwa kuwa kitatoa mafunzo, huduma za kitaaluma, na msaada wa masoko kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kutoa ufumbuzi wa kudumu kwa changamoto zinazowakabili wakulima.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post