Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADEREVA WASHAURIWA KUPATA MAFUNZO YA UDEREVA

 


Na Okuly Julius-Dodoma

MKUU wa chuo cha mafunzo ya udereva cha Wide Institute of Driving jijini Dodoma, Faustine Matina ameishauri serikali kuweka mikakati ya kukomesha ajali nchini ikiwemo mafunzo maalum ya mara kwa mara kwa madereva wa serikali ambao wamekuwa wakilalamikiwa kutozingatia sheria za usalama barabarani.


Matina, amesema hayo Leo Agosti 19,2023 jijini Dodoma, wakati wa mafunzo kwa madereva wa malori wasiokuwa na vyeti vya udereva ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Jeshi la Polisi.


Mapema mwaka huu waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Hamad Yusuf Masauni, alitoa maagizo kwa jeshi la polisi kufanya ukaguzi wa leseni za madereva wa malori na mabasi ili kukomesha ajali zilitokea mfululizo katika maeneo mbalimbali nchini.


Masauni, aliagiza madereva wote ambao wanaleseni lazima wawe na vyeti vya mafunzo ya udereva kutoka vyuo vinavyotambulika na atakaye kosa sifa hatua zichukuliwe.


“Kazi ya vyuo vya udereva ni kuhahakikisha kuwa tunaandaa madereva bora ili kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani kutokana na uzembe hapa leo tunao madereva wa malori ambao wanaleseni lakini hawana mafunzo ya udereva tunawafunisha sheria za usalama barabarani, utii wa sheria bila shurti kuwa watiifu wanapokuwa njiani na vyombo vya moto”amesema Matina


Aidha, amesema pamoja na serikali kutoa maagizo hayo utaratibu huo unapaswa kuwa endelevu ili kusaidia madereva wote ambao wanaendesha vyombo vya moto bila kuwa na mafunzo.


“Tunaomba hili liwe endelevu ili madereva wote wapate mafunzo na kukomesha ajali zinazotokea kwa makosa ya kibinadamu lakini pia serikali iandae program maalum kwa ajili ya madereva wa serikali ambao wamekuwa wakilalamikiwa namna wanavyoendesha vyombo vyao hawazingatii sheria za usalama barabarani”amesema Matina


Amesema madereva ni binadamu ambao wanahitaji kupata muda wa mafunzo ya kukumbushwa wajibu wao mara kwa mara kwakuwa mambo mengi yanabadilika kila siku hivyo serikali inapaswa kuzingatia ushauri huo kwa ajili ya kukomesha ajali.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa madereva Tipa Dodoma (UMATIDO) Praygod Malle,alikishukuru chuo hicho kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani kwa kutoa mafunzo hayo.


“Tunaishukuru serikali yetu kwa kutoa maagizo ambayo yamewezesha leo madereva kupata mafunzo ambayo yatakwenda kupunguza tatizo la ajali nchini ambazo nyingi zimekuwa zikitokea kwa makosa ya kibinadamu”amesema Malle


Hata hivyo, ametoa wito kwa madereva wote ambao wanaendesha vyombo vya moto bila kuwa na mafunzo kuchangamkia fursa hiyo ili kuepuka kusumbuliwa na mamlaka katika oparesheni mbalimbali za ukaguzi wa leseni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com