Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPONGEZWA KWA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO YA MIGONGANO BAINA YA BINADAMU NA WANYAMAPORI

Na  John I. Bera  
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zake za Uhifadhi zilizopo ndani ya mikoa ya kusini pamoja na halmashauri za wilaya kwa jitihada zake kubwa za kupambana na changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori.


Ametoa pongezi hizo Agosti 10, 2023 wakati akifungua warsha ya utambulisho wa mradi wa kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika Ukanda wa Ruvuma Mkoa wa Lindi katika Wilaya ya Liwale na Ruvuma Wilaya za Namtumbo na Tunduru.


"Migongano hii inahatarisha maisha ya wananchi na mali zao na usalama wa chakula kwa mfano kwa mwaka mmoja pekee 2022/ 2023 wanyamapori wakali na waharibifu wamesababisha uharibifu wa takriban jumla ya ekari 1,0724.05 za mazao mbalimbali." amesema.


Aidha, amesema Serikali ina matarajio makubwa na mradi huo ambao mara utakapoanza kutekelezwa utasaidia kupunguza au kumaliza changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika mikoa na wilaya husika.


"Hivyo, ni matumaini yetu kuwa mradi huu utawezesha mambo ya msingi ambayo yatatatua changamoto hii ikiwemo vitendea kazi na matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu", ameongeza.


Wakati huo huo, Kanali Laban ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa Shirika la Ujerumani (GIZ) kwa kukubali kuleta mradi huu katika ukanda wa Ruvuma.

"Mradi huu umekuja wakati muafaka kutokana na ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo hayo. Nafahamu kuwa mradi huu utatekelezwa katika wilaya za Namtumbo, Tunduru na Liwale lakini niwaombe tuweke mpango mahsusi wa baadaye ili kupeleka mafanikio yatakayopatikana kutokana na Mradi huu kwenye mikoa na wilaya nyingine zenye changamoto hii", amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Bi. Antonia Raphael amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani katika kutekeleza Mradi huo ni muendelezo wa jitihada za Serikali katika utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika maeo mbalimbali nchini.


Vilevile, amesema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itahakikisha kuwa Mradi huo unatekelezwa kikamilifu ili kuepusha madhara kwa wananchi na mali zao kutokana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori hususan katika Mikoa ya Ruvuma na Lindi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu hiyo kutoka Shirika la GIZ, Bw. Jens Bruggemann amesema, wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto hiyo ili kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo wanakuwa na mtazamo chanya juu ya wanyamapori na sio kero katika maisha yao.


Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ushirikiano na Shirika la GIZ kutoka Ujerumani imekuja na mradi huo utakao saidia kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori utakao tekelezwa katika mikoa ya Lindi na Ruvuma.

Mradi huo ni matunda ya ushirikiano kati ya Serikali ya Ujerumani na Serikali ya Tanzania ambao utatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Shirika la GIZ la Ujerumani kwa kuhusisha Taasisi za TAWA, TFS TANAPA, TAWIRI, mikoa na wilaya husika pamoja na wadau wengine wa Uhifadhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com