Na Dotto Kwilasa, DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa wito kwa wananchi wa Mikoa ya Dodoma na Singida kutembelea mabanda ya maonesho ili kujifunza mbinu na teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji bora kutoka kwa wakulima na wafugaji wenzao, Taasisi za Kitafiti, bodi za mazao na mashirika mbalimbali ya umma, watu binafsi kwakuwa ni darasa la kujifunza .
Wito huo umetolewa Agosti 2, 2023 wakati akizundua wa Maonyesho ya 15 sherehe za nanenane Kanda ya kati Mwaka huu katika viwanja vya nane nane Nzuguni Jijini Dodoma.
"Utaratibu huu unatoa fursa kwa wananchi wanaotembelea mabanda ya maonesho kujifunza mbinu na teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji bora kutoka kwa wakulima na wafugaji wenzao, Taasisi za Kitafiti, bodi za mazao na mashirika mbalimbali ya umma na watu binafsi. Hivyo, nawapongeza sana wote mliojiandaa na kujitolea kushiriki katika maonesho haya yenye mafunzo mengi "ameeleza Senyamule
Aidha, Mhe. Senyamule amesema Serikali imepanga kubadilisha kilimo kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha kibiashara ambapo amesema mabadiliko hayo yanafanyika kwa kuzingatia malengo ya kitaifa kama yalivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo 2015 -2025, Sera ya Kilimo ya Mwaka 2013 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2021-2025.
"Juhudi hizi za Serikali, zinatarajiwa kusaidia wakulima kuanzisha Viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo na Mifugo ili kuyaongezea thamani kabla ya kuingizwa sokoni. Kwa kuwa ni rahisi kwa Serikali kusaidia wazalishaji wakiwa kwenye vikundi/ ushirika/ umoja, hivyo nawahamasisha wazalishaji kujiunga katika vikundi ili iwe rahisi kupewa ruzuku au mikopo yenye riba nafuu ambayo itasaidia kuboresha shughuli za uzalishaji na hivyo kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla."amesisitiza Senyamule
Katika hatua nyingine, Mkuu Mkoa huyo amewaagiza wananchi kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo kwa kuepuka matumizi mabaya ya kemikali, kuacha ukataji miti ovyo, kuchoma moto, ufugaji holela, kulima kwenye vyanzo vya maji na kuzingatia matumizi sahihi ya zana za kilimo na pembejeo.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Peter Selukamba amesema pato la Mkoa wa Singida linategemea wakulima, wafugaji na wavuvi hivyo maonesho hayo yatakuwa chachu ya maendeleo kwani yanatoa ujuzi na elimu za teknolojia wezeshi.
Amesema shughuli za kilimo zinatekelezwa kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha ziada kwa matumizi ya chakula na biashara kupitia mbinu mbalimbali ikiwani pamoja na kilimo cha umwagiliaji kinachorahisisha kilimo kwa mwaka mzima.
Social Plugin