MARYPRISCA AIPONGEZA DAWASA KUIBUA MRADI WA MAJITAKA MBEZI BEACH



NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

NAIBU Waziri wa Maji Mhe.Maryprisca Mahundi amefanya ziara ya kutembelea Mradi wa ujenzi wa mfumo wa Majitaka Mbezi Beach ambapo ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuona umuhimu wa kuwepo kwa mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara hiyo leo Agosti 21,2023 Jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mahundi amesema mradi huo utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 52 mpaka utakapokamilika ndani ya miezi 18.

"Mpaka sasa mradi wa huu wa kuondosha majitaka katika jamii na kwenda kuyatunza katika mazingira ambayo yanaweza yakarudi tena kwenye mzunguko wa matumizi, umeanza kwa kasi na utekelezaji upo ndani ya muda na Serikali kupitia DAWASA imeshatoa malipo ya awali ya bilioni 7 ili kuhakikisha utekelezaji unakwenda kwa kasi". Amesema Mhe.Mahundi.

Aidha amesema "Hii ni moja ya jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia za kuwekeza fedha za kuboresha maisha ya Watanzania na tayari Wizara tumeshasaini mkataba mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya majitaka na usafi wa mazingira katika mikoa mingine,"

Pamoja na hayo amesema kuwa miradi hii ambayo ameitembelea ikiwemo ya ujenzi wa vituo vya huduma za usafi wa mazingira kwa jamii na ujenzi wa mfumo wa kukusanya majitaka Mbezi Beach ni miradi ya mfano nchini ambayo imelenga kuboresha Usafi wa Mazingira na afya za wakazi Dar es Salaam.

"Nimetembelea utekelezaji wa miradi hii na nimeona ufanisi wa hali ya juu. Nitoe wito kwa Mamlaka nyingine nchini kujifunza kwa DAWASA namna ya kubuni na kutekeleza miradi yenye kuakisi hali halisi ya uboreshaji wa usafi wa mazingira katika maeneo yao," ameeleza Mhandisi Maryprisca.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Shabani Mkwanywe amesema kuwa Mamlaka imejipanga kuhakikisha inatekeleza miradi ya usafi wa mazingira yenye uwezo wa kuendana na ongezeko la kiwango cha maji kinachozalishwa pamoja na ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

"DAWASA tunatekeleza miradi ya mkakati ya Usafi wa Mazingira inayohusisha ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kuchakata majitaka katika maeneo ya Mbezi Beach, Buguruni pamoja na kukarabati mabwawa ya Kurasini ili kuongeza ufanisi," amesema.

Mhandisi Mkwanywe amesema kuwa kwa sasa tunaongeza nguvu kwenye miradi ya uondoshaji majitaka ambayo ni matokeo ya uboreshaji wa huduma ya Majisafi. Hivyo mradi huu wa Mbezi beach, ni wa mfano na unatekelezwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kwa bilioni 120. Katika awamu ya kwanza, mradi unagharimu bilioni 52, ambapo mpaka sasa bilioni 7 malipo ya awamu ya kwanza yameshalipwa.

"Mradi huu ni wa kisasa ambao utahusisha kazi ya kukusanya majitaka toka majumbani na baada ya kuchakatwa katika mtambo wa kisasa utakaojengwa Mbezi Beach, na pamoja na maji, mtambo utazalisha gesi asilia na mbolea," ameeleza Mhandisi Mkwanywe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post