MBUNGE wa Viti Maalum Fatma Toufiq amesema suala la ukatili wa wanawake na watoto na ulawiti kwa watoto wa kiume limekithiri kwa kiasi kikubwa na hivyo kutoa rai kwa viongozi na jamii kwa ujumla kukemea suala hilo na kuchukua hatua.
Akizungumza Agosti Mosi Jijini Dodoma katika kikao cha kawaida cha Baraza la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),Wilaya ya Dodoma Mjini,Mbunge Fatma amesema kwa sasa suala hilo limekithiri sana na hivyo kupelekea wengine kuathirika kisaikolojia.
“Tunaona kwa sasa kumekuwa na matukio mabaya hasa kwa watoto wa kike ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili na watu wao wa karibu ,wanawake wanakatwa mikono,wanatolewa macho,wanauawa,wanapigwa na hii inawaathiri sana watoto na kupata madhara zaidi,
“Viongozi wenzangu tukemee suala hili,jamii pia ikemee na tuchukue hatua ya kupambana na ukatili huutuwalinde watoto wetu kwa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili na wasiogope kusema,”amesisitiza.
Aidha,amewaasa wazazi kulea watoto wao katika maadili mema kwa kumuogopa Mungu ili waje kuwa wazazi wema.
Akizungumzia suala la uwekezaji wa Bandari ,mbunge huyo amesema kumekuwa na upotoshaji mkubwa.
“Hii ni vita ya kiuchumi,Rais wetu Samia Suluhu Hassan ana nia ya kuboresha utendaji kwa kutafuta wawekezaji wenye utaalam katika uendeshaji wa bandari ,
“Niwaombe wanawake wenzangu tuseme mazuri anayofanya Rais Samia ili wananchi watambue juhudi zake katika kuleta Maendeleo ya nchi yetu na Mungu akijaalia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tuhakikihe ushindi mnono unapatikana na 2025 miaka mitano mingine kwa Rais Samia ili aendeleze maono aliyonayo,”amesema.
Social Plugin