Na. Veronica Mwafisi-Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka wananchi kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa na watu wasio wema kuhusiana na ndege ya Rais Gulf Stream (G550) kushikiliwa nchini Dubai.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ndege za Serikali katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Mtu anaweza kuzusha jambo na likawapotezea muda mwingi wananchi badala ya kufanya mambo ya maendeleo, kwa mfano uzushi kuhusiana na ndege ya Rais Gulf Stream (G550) kuzuiliwa Dubai, nataka niwahakikishie Watanzania kuwa ndege hiyo ipo sehemu husika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Terminal 1 VIP, jijini Dar es Salaam kwenye eneo ambalo Wakala wa Ndege za Serikali wanalitumia na yeyote anayepita barabarani ataiona,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Mhe. Simbachawene amesema yeye akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya Utawala Bora ameona aliweke wazi jambo hilo, lililoleta taharuki ili kuwaondoa hofu Watanzania na uvumi huo ulioenea, hivyo lisiwapotezee muda wao na kuwahakikishia wanaovumisha hayo kwa nia ovu wanaweza kwenda kupata uhakika wa uwepo wa ndege hiyo ambapo ameongeza kuwa Viongozi wanasafiri kama kawaida kwa kutumia ndege hiyo.
Aidha, Mhe. Simbachawene ametoa wito kwa Wajumbe wa Bodi hiyo kushirikiana na Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali ili kuiwezesha Wakala hiyo kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Ni matarajio yangu kuwa Bodi hii itasimamia vema utendaji wa Wakala hii ili kuleta tija kwa maendeleo ya taifa kama inavyosisitizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ndege za Serikali, Prof. Mhandisi, Idrissa Mshoro amemuahidi Mhe. Simbachawene kuwa, yeye pamoja na Wajumbe wa Bodi hiyo kwa kushirikiana na Menejimenti ya TGFA watatekeleza yote ambayo ameyaelekeza kwani wanafahamu kwa kina maono makubwa ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika katika kuharakisha maendeleo ya nchi katika kuhakikisha uwepo wa usafiri madhubuti.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) Capt. Budodi Budodi amesema Menejimenti ya Wakala inamhakikishia Mhe. Simbachawene kuwa wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na maelekezo ya Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ndege za Serikali ili kufikia malengo ya uanzishwaji wa Wakala hiyo.
Social Plugin