Na Mariam Kagenda - Muleba
Zaidi ya Wananchi 4,570 wa kata ya Bureza wilayani Muleba mkoani Kagera wameondokana na changamoto ya uhaba wa huduma ya maji iliyokuwa ikiwakabili muda mrefu baada ya Mwenge wa uhuru kuzindua mradi wa maji Butembo wenye thamani ya shilingi milioni 986.
Wakizungumza baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo baadhi ya wananchi wa kata ya Bureza wamesema kuwa ilikuwa ikiwalazimu kutumia zaidi ya masaa 4 kwenda mtoni kuchota maji na wakifika wanakutana na foleni ambapo wakati mwingine walikuwa wananunua ndoo ya maji kwa shilingi mia tano.
Wamesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwakumbuka na kuleta mradi wa maji Butembo kwani wanatumia muda waliokuwa wanafata maji kufanya shughuli nyingine za uzalishaji.
Awali wakati akisoma taarifa ya mradi huo kabla ya kuzinduliwa na mwenge wa uhuru Meneja wa wakala wa maji na usafi wa Mazingira vijijini RUWASA Mhandisi Patrice Jerome amesema kuwa kiasi chote cha fedha kimegharamiwa na fedha za lipa kwa Matokeo chini ya program ya uendelevu na usafi wa mazingira kijijini.
Mhandisi Jerome amesema kuwa mradi huo adi kukamilika umesimamiwa na Ruwasa ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya mtambo wa maji,Uzio, ufungaji wa pampu 2 za maji zenye uwezo wa mita za ujazo 16.9m ,ujenzi wa vituo 22 vya kuchotea maji pamoja na uchimbaji wa mtaro wa maji.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Abdalla Shaib Kaimu wakati akizindua mradi huo amesema kuwa mwenge wa uhuru umekagua nyaraka na umetembelea mradi huo na kuona kazi kubwa na nzuri iliyofanywa katika mradi huo mkubwa na kulidhishwa na mradi.
Ameongeza kwa kusema kuwa lengo la serikali ni kumtua mama ndoo kichwani na inatumia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo hivyo wananchi wanatakiwa kuitunza .
Aidha mwenge wa uhuru ukiwa wilayani Muleba umekagua ,Kuzindua na kutembelea jumla ya miradi 8 ya maendeleo..
Social Plugin