Meneja wa Sekta isiyo rasmi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Rehema Chuma (kushoto) akimsikiliza Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga, Theresia Makyao mara baada ya kutembelea banda na NSSF wakati wa kongamano la Wanawake na Manunuzi ya Umma, linalofanyika jijini Tanga
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeshiriki na kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa washiriki wa kongamano la Wanawake na Manunuzi ya Umma, linaloendelea jijini Tanga.
Akizungumza wakati wa kongamano hilo Meneja wa Sekta isiyo rasmi, Rehema Chuma ambaye alikuwa miongoni mwa waliotoa mada katika kongamano hilo lililoanza tarehe 23 Agosti, 2023, amesema kupitia kongamano hilo NSSF imetoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi ambayo imebeba kundi kubwa.
Kundi hilo kubwa ambalo sekta isiyorasmi ni kama vile wakulima, wafugaji, wavuvi, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine wote ili waweze kujiunga na kuchangia katika Mfuko kwa maisha yao ya sasa na baadaye.
Lengo la kongamano hilo ni kueleza fursa za biashara zinazoambatana na mradi wa bomba la mafuta Afrika Mashariki (EACOP) hivyo mradi huo ni fursa kwa NSSF kupata wanachama wapya ambao watapata ajira za moja kwa moja na wale watakaonufaika na ajira za muda pamoja na wanufaika wengine kama vile mama lishe na bodaboda ambao wataweza kujiunga na kuchangia katika Mfuko.
Katika kongamano hilo, NSSF licha ya kutoa elimu ya hifadhi ya jamii pia itaeleza fursa mbalimbali zinazopatikana zikiwemo za nyumba na viwanja ambazo zinauzwa kwa bei nafuu.