MKUU wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba akizungumza wakati akifungua kikao cha nusu mwaka cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu. |
MKUU wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba akizungumza wakati akifungua kikao cha nusu mwaka cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba, amehimiza jamii kutilia mkazo lishe bora kwa watoto hususani wa chini ya miaka mitano, ili kuwa na kizazi chenye afya na tija katika uzalishaji na utoaji huduma.
Ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua kikao cha nusu mwaka cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa amesema ombwe katika masuala ya lishe linaanzia utotoni pale watoto wanapokosa lishe bora hivyo kuathiri ukuaji na afya zao.
‘’Tukiwaacha wakue hovyo hovyo ndio baadaye wataleta matatizo kwenye nchi. Tunasema hakuna madaktari wazuri, hakuna wakandarasi wazuri…ni kwa sababu hatukuwangalia wakati wakiwa watoto walikuwa wanakula chakula gani,’’ amesema.
Amesema hitihada za uboreshaji lishe kwa watoto zinapaswa kutilia mkazo kwa wazazi na walezi kutambua aina ya chakula, kazi na umuhimu wake kwa mtoto.
‘’ Hapa suala lisiwe mtoto kula kwa lengo la kushiba, bali kutambua chakula kinakwenda kufanya kazi gani mwilini,’’ amesema.
Kindamba amesema pamoja na changamoto zilizopo, mkoa huo umefanikiwa kuongeza wastani wa jumla kwa Shilingi 100 zinazotengwa na halmashauri kwa kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano, kutoka Shilingi 794.3 katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2022 kufikia Shilingi 1,272.3 kwa Januari hadi Juni, 2023.
Pia amesema kumekuwepo ongezeko la asilimia ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe kutoka 57.7 kwa Julai hadi Disemba, 2022 kufikia 96.79 katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2023.
Mkuu wa mkoa amesema lishe bora kwa jamii ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja zote zikiwemo afya, elimu, biashara, kilimo na uchumi.
Hivyo, amesema ni pale ambapo athari za lishe duni na utapiamlo zitakazodhibitiwa au kutokomezwa, malengo ya maendeleo katika nyaja hizo yatafikiwa kwa ufanisi.
Social Plugin