Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUWAKUTANISHA WADAU KUJADILI UTEKELEZAJI MAGEUZI MAKUBWA YA ELIMU NCHINI



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ,akisalimiana na Wanafaunzi wa shule ya Sekondari Uru mara baada ya kuwasili katika Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule hiyo iliyopo mkoani Kilimanjaro.

Na.Mwandishi Wetu-KILIMANJARO

SERIKALI imesema Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na mabadiliko ya Mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu itakapopitishwa itakutana na wadau wote wa Elimu zikiwemo Taasisi zote za Dini pamoja na Sekta binafsi kujiandaa kutekeleza kwa pamoja mageuzi makubwa ya elimu nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Mkoani Kilimanjaro alipokuwa akizungumza katika Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani humo ambapo amesema katika kutekeleza mageuzi hayo serikali inawahitaji sana wadau ili kwenda sambamba katika mageuzi hayo.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa mchakato mzima wa ukusanyaji maoni ulihusisha wadau mbalimbali ambao walitoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa rasimu hizo, hivyo serikali imeona umuhimu kwa wadau hao kushiriki kuweka mikakati ya utekelezaji.

“Rasimu ya Mapitio ya Sera na mabadiliko ya Mitaala zitakapopitishwa rasmi na mamlaka husika na kuwa tayari kwa ajili ya utekelezaji, tutakutana tena na kushirikisha taasisi zote za dini za Kiisilamu na Kikristo pamoja na sekta binafsi kuona ni vipi tunajiandaa kwa pamoja katika kutekeleza mageuzi haya ili na nyie mchangie katika hilo kwa sababu tunawahitaji sana” ameelezea Waziri Mkenda.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa kazi ya kufanya mabadiliko ya Mitaala imefanyika kwa kipindi cha miaka miwili kwa kushirikisha wadau ambapo amesema maandalizi ya Mtaala wa somo la dini umeshirikisha madhehebu yote ambayo kwa pamoja yalikubaliana kwamba ni mtaala sahihi, huku akiwataka wadau kutembelea tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania ili waweze kuiona mitaala hiyo pendekezwa na kama kuna lolote lisilo sawa.

Kuhusu kuanza kwa Mtaala wa masomo ya amali Waziri huyo amesema unaweza kuanza kutekelezwa katika shule tisa za ufundi zilizopo nchini ambazo tayari zilishatembelewa, kufanyiwa tathimini pamoja na kutengewa fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi uhandisi. Amezitaja shule hizo kuwa ni Tanga, Moshi, Ifunda, Iyunga, Musoma, Mtwara, Bwiru, Shinyanga na Chato kwamba utaratibu umewekwa kuwawezesha wahitimu kuendelea na elimu ya juu.

Akizungumzia uwekezaji katika sekta ya elimu amesema katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita fedha nyingi zimetolewa ambazo zimewezesha ujenzi na ukarabati wa miundombinu ambayo imetoa fursa kwa watoto wanapomaliza elimu ya msingi kujiunga kidato cha kwanza kwa mara moja tofauti na zamani ambapo ililazimika kusubiri awamu ya pili na pia hakuna tena zoezi la wazazi kulazimishwa kutoa michango ya ujenzi ili kuwezesha watoto kupata madarasa.

“Hiki ni kiashiria cha namna uwekezaji mkubwa unavyofanywa na serikali, tunaona fedha zinatengwa, shule zinajengwa zinakamilika wanafunzi wanaingia hakuna tena kukimbizana na wazazi kuhusu michango, ingawa kwa hiari wazazi wanaweza kuchangia maendeleo ya elimu” amefafanua Waziri huyo.

Kwa Upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo la Moshi, Mhashamu Baba Askofu Ludovick Minde amemshukuru Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda kwa kusimamia vyema sekta ya elimu na maono ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu na ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kuchangia katika uchumi wa taifa.

Kwa upande wake Katibu wa Elimu Msaidizi Jimbo Katoliki la Moshi, Padri Peter Asantebwana amesema kuwa katika mabadiliko ya mitaala wao kama wadau wakubwa wa elimu wanaiomba serikali isiwasahau katika mageuzi hayo kwa kuwasaidia kuwapatia vitabu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwemo vifaa vya maabara ili nao waweze kutekeleza kwa ufanisi na weledi katika kuwapatia elimu bora watoto wa kitanzania.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ,akisalimiana na Wanafaunzi wa shule ya Sekondari Uru mara baada ya kuwasili katika Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule hiyo iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akiteta na Viomgozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akiteta jambo na Askofu Mkuu wa Jimbo la Moshi, Mhashamu Baba Askofu Ludovick Minde wakati wa Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati wa Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Askofu Mkuu wa Jimbo la Moshi, Mhashamu Baba Askofu Ludovick Minde,akizungumza wakati wa Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Mkuu wa shule ya Uru Mwalim Peter Osoki,akitoa taarifa wakati hafla ya Maadhimisho ya Miaka ya 50 Jubilei ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,(hayupo pichani) wakati wa Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akimkabidhi cheti Mwanafunzi wa kidato cha 4 wa Shule ya Sekondari Uru Sekondari iliyopo Mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya Shule hiyo.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akipokea Tuzo kutoka kwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Moshi, Mhashamu Baba Askofu Ludovick Minde wakati wa Hafla ya Jubilei ya miaka 50 ya shule ya Sekondari Uru iliyopo mkoani Kilimanjaro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com