SERIKALI KUWEZESHA MJADALA WA MILA POTOFU YA KUWEKEZA MKE TUMBONI MWA MAMA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akijibu Swali la Mbunge wa Viti Maalum Mary Azan Mwinyi Bungeni leo Agosti 31,2023 jijini Dodoma.

Na WMJJWM, Dodoma

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Wataalamu wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii ngazi ya Jamii kuandaa majukwaa ya kuongoza majadiliano kuhusu mila potofu ya kuwekeza mke akiwa tumboni.

Akijibu swali la Mhe. Mary Azan Mwinyi, Bungeni Dodoma leo Agosti 31, 2023 aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama hasa Manyara na Arusha, Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali imeandaa utaratibu wa kuendesha majadiliano yatakayokuja na jumbe mahsusi ili kutumika kwenye majukwaa tofauti, kutoa elimu ikiwa pamoja na nyumba za ibada.

"Serikali inatambua kuwa kuna mila zenye faida ambazo zinapaswa kuendelezwa na mila zenye kuleta madhara ikiwemo mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama. Mila hii ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kihisia, ndoa za utotoni na inamnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika." amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Wizara imeandaa mwongozo wa kuendesha majadiliano unaojulikana kama "Mwongozo wa Taifa wa Uendeshaji Majadiliano Kuhusiana na Mila na Desturi zenye Madhara kwa Jamii wa mwaka 2022".

Amebainisha kwamba, majadiliano hayo yanakuwa ni jumuishi yanayohusisha viongozi wa Mila, Viongozi wa Dini, Wazee maarufu na wataalamu waliopo katika ngazi ya jamii ili kuja na ujumbe mahsusi wenye lengo la kutokomeza mila zenye madhara ikiwa pamoja na kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post