Na Alex Sonna-SINGIDA
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), imetaja mikakati yake ya kuimarisha upatikanaji wa maji na uondoshaji wa majitaka ikiwamo kutekelezwa kwa mradi wa maji wa Miji 28 unaogharimu Sh.Bilioni 45.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 5, 2023 mjini Singida, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), Bw.Sebastian Warioba, amesema kuna mradi mkubwa unaoendelea kwasasa ambao umeanza utekelezaji mwezi Aprili, 2023 kupitia mradi wa Miji 28 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.
Amesema mradi huo utaongeza upatikanaji wa maji na kuwafikia wateja kwa asilimia 90 kwenye Manispaa ya Singida.
“Kwa manispaa ya Singida tuna takribani Sh.Bilioni 45 za mradi wa miji 28, tunashukuru serikali mkandarasi ameanza kazi na anafanya kazi maeneo yote ya mradi,”amesema Bw.Warioba
Amesema kuna miradi mingine wanategemea kutekeleza kwa kupata fedha serikali kuu ili kuwafikia wananchi ambao hawajafikiwa na mtandao wa maji.
“Manispaa tuna kata 18 tumeshafikia kata 16 ambapo kuna baadhi hazijafikiwa kwa ukamilifu na zingine mbili hatujazifikia kabisa, tumewasilisha andiko Wizara ya Maji ili kupata fedha zaidi ya Sh.Bilioni tatu,”amesema.
Amebainisha kuwa Mamlaka hiyo ina wateja wa maunganisho ya maji safi 18,000 na imewafikia kwa asilimia 78.
“Eneo tunalohudumia ni Manispaa ya Singida pamoja na miji mingine saba nje ya Manispaa ambayo ni Buguno, Njia panda, Ikungi, Sepuka, Irisia, Puma na Makiungu ambapo tumewafikia wateja kwenye miji hiyo kwa asilimia 68,”amesema.Bw.Warioba
Hata hivyo, amesema suala la upotevu wa maji lipo kwa asilimia 31 na kuna mikakati ya kukabiliana na hali hiyo.
“Upotevu unachangiwa na vitu mbalimbali moja wapo ni matumizi ya yasiyosahihi au wizi wa maji, pia inasababishwa na uchakavu wa miundombinu, tunachofanya kuna maeneo tumefanya ukarabati, kubadilisha mita za zamani zinazosoma chini ya kiwango,”amesema.
Amesema mapema mwaka huu mamlaka hiyo imepata mita zaidi ya 20,000 za maji ambazo zinatumika kubadilisha na kuunganisha wateja, huku ikipewa mabomba ya zaidi ya sh. Milioni 300.
“Tunatarajia kupata mabomba mengine ya zaidi ya Sh.Bilioni moja ili kubadilisha na kuunganisha kwa wateja ili kuondokana na upotevu wa maji,”alisema.
Kuhusu uondoshaji wa majitaka, amesema Manispaa hiyo haikuwa na huduma hiyo na kuanzia mwaka huu wameanza utekelezaji wa mradi wa uondoshaji majitaka ambapo wameanza na kujenga mabwawa eneo la Manga.
“Mabwawa haya yatakapokamilika mwishoni mwa mwaka 2024 tunategemea makazi ya wananchi yatakuwa salama kwa kuondosha majitaka na kupeleka kwenye mabwawa na maji hayo yatatibiwa na baadaye yataweza kutumika kwa manufaa ya kiuchumi ya wakazi wa hapa kama vile shughuli ya kilimo,”amesema.
Kadhalika, amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Maji wameanza upembuzi yakinifu na kufanya tathmini ya athari za mazingira ili kutekeleza mradi kubwa wa majitaka wa kuweka mtandao kwenye makazi ya watu na kuongeza mabwawa ya majitaka.
“Wiki ijayo tunategemea mtaalamu mshauri atafika ili kupita maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuhuwisha study iliofanyika mwaka 2015 ili zitafutwe fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu maana wakati ule mradi ulikuwa wa gharama ya zaidi ya Sh.Bilioni 45 kwa kuwa muda umepita mrefu wizara imeona ufanyike upya ili kuendana na hali halisi ya sasa,”amesema.
Ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pindi inapotokea hujuma kwenye maeneo ya miradi na miundombinu.
Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Sebastian Warioba akiwa kwenye Ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka eneo la Manga Manispaa ya Singida. Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi MS. Nangai & pentels Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 1.765
Social Plugin