TEA KUTUMIA BILIONI 8 MIRADI YA ELIMU MWAKA WA FEDHA 2023/24


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) Bi Bahati Geuzye akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma

******************

Mamlaka ya Elimu Tanzania imepanga kutumia kiasi cha Sh. Bilioni 8 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini ili kusaidia upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini..

Akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa Habari, Agosti 10, 2022 katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma, Mkurugenzi MKuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye amesema kiasi hicho cha fedha kitatumika kufadhili miradi 82 katika shule 81 zikiwemo shule 48 za msingi na 33 za sekondari katika maeneo mbali mbali ya Tanzania Bara.

Ametaja miradi itakayofadhiliwa kuwa ni ujenzi wa madarasa 82, matundu ya vyoo 336, mabweni 10, ujenzi wa maabara 18 za masomo ya sayansi na nyumba za walimu 32 na hivyo kuwanufaisha wanafunzi 39,484 na walimu 169 katika shule za msingi na sekondari.

Aidha katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 Mfuko wa Elimu wa Taifa utatoa ufadhili kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika taasisi moja ya elimu ya juu Tanzania – Zanzibar ambapo kiasi cha Sh. Milioni 300 zitatumika katika utekelezaji wake.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA ametumia fursa hiyo kushukuru wadau wanaochangia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambapo katika mwaka wa fedha wa 2022/23 miradi yenye thamani ya Sh. Milioni 404 ilifadhiliwa na wadau mbali mbali wa elimu

Wadau waliochangia ni pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), BRAC Maendeleo Tanzania, Taasisi ya Asilia Giving, Taasisi ya Flaviana Matata, Taasisi ya SAMAKIBA, CAMARA Education Tanzania na Kampuni za Sayari Safi na Dash Industries Ltd.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) Bi Bahati Geuzye akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma

Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi Bahati Geuzye katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post