Na Dotto Kwilasa, DODOMA
Serikali kupitia Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imesema itaendelea kusimamia shughuli za uzalishaji wa mbegu na biashara ya mbegu ili kuwahakikishia wakulima na wadau wengine kuwa mbegu wanazouziwa zina lebo ya ubora ya TOSCI na ni mbegu sahihi kwa matumizi.
Hayo yameelezwa leo Agost15,2023 Jijini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Patrick Ngwendiaga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya habari- Maelezo kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya baraza hilo kwa mwaka 2023/2024.
Amesema TOSCI yenye makao makuu yake mkoani Morogoro, ina ofisi tano (5) za Kanda ambazo husimamia masuala yote ya uthibiti na udhibiti wa ubora wa mbegu katika Kanda husika ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Njombe), Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kanda ya Kusini (Mtwara), Kanda ya Magharibi (Tabora).
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa ili kufanikisha majukumu yake, TOSCI husajili wafanyabiashara/wazalishaji wa mbegu,kufanya majaribio ya utambuzi wa aina mpya za mbegu pamoja na Kufanya majaribio ya umahiri wa aina mpya za mbegu.
"Tumeanza pia usajili aina mpya za mbegu zilizoidhinishwa kwa ajili ya uzalishaji wa kibiashara baada ya kukidhi vigezo vya usajili,kukagua mashamba ya mbegu yanayosajiliwa,
kuchukua sampuli za mbequ kwa lengo la kupima ubora wake na kupima ubora wa mbegu kwenye maabara za mbegu,"amesema
Kuhusu utekelezaji wa majukumu yake, amesema Katika Mwaka wa fedha 2022/2023 TOSCI ilitengewa Shilingi bilioni 10.6 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi kwa ujumla na kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara ya mbegu 1,832 na kusajili aina 1,031za mbegu.
Amefafanua kuwa kupitia fedha hizo Taasisi hiyo imefanya majaribio ya utambuzi wa mbegu aina 49 na umahiri wa aina mpya za mbegu 18 ikiwa ni pamoja na usajili na ukaguzi wa mashamba ya mbegu 1,554.
Akizungumzia mafanikio ya TOSCI amesema,"Tumefanikiwa kwenye Ongezeko la mbegu zilizothibitishwa ubora kitaifa na kimataifa kwenye mazao ya mahindi, mpunga, mtama, alizeti, mbegu za maboga, maharage, pamba, choroko, mbaazi, karanga, ufuta, ngano, kunde, njugu mawe, ulezi, tumbaku na maharage ya soya;
Ongezeko la matumizi ya lebo za ubora: Matumizi ya lebo za ubora za TOSCI kumesababisha kupunguza tatizo la uwepo wa mbegu feki au zilizo na ubora hafifu,"amesema