Mkuu wa wilaya ya Mbulu Kheri James ameongoza msafara wa kukagua mradi wa kuvuna ukungu na maji uliopo mkoani Manyara wilaya ya Mbulu.
Ziara hiyo ilifanyika Leo Agost 23,2023 ikiongozwa na mkuu wa wilaya akiambatana na wakurugenzi, wataalamu wa mradi pamoja na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu na Mbulu mji.
Mkuu wa Wilaya Kheri alisema kuwa wilaya ya Mbulu ni miongoni mwa wilaya ambayo inanufaika na mradi wa uvunaji wa maji kupitia ukungu.
"Kama ilivyotaratibu zetu viongozi inabidi kujengewa uwezo ni namna gani mradi huu utafanyika na mazingira ya mradi yatakuwaje, kwa busara ya kawaida Leo viongozi wote na watumishi kwa uwakilishi tumeona tufike hapa Babati ambapo mradi huu unafanya kazi vizuri, kwa tija kubwa sana na unasaidia upatikanaji wa maji safi kwa ajili ya wanafinzi wa shule ya sekondari Qameyu,matumizi ya laboratory na matumizi mengine ambayo shule itahitaji." Alisema Mkuu wa Wilaya.
Mheshiwa Mkuu wa Wilaya aliendelea kusema kuwa jitihada kubwa zinafanywa na serikali katika kuhakikisha maji safi na Salama yanapatikana, jitihada hizi zinafanywa na serikali pamoja na wadau, na wadau wanaongeza nguvu kwa sababu kubwa moja, hakuna namna tutaleta maendeleo ya watu wetu bila maji safi na Salama.
"Mradi sasa unapokwenda kuanza tumeshajifunza baadhi ya mambo ya kuanza nayo wakati wa kuanza, lakini mambo ya kufanya wakati wa mradi unaendelea, na mambo ya kufanya ili kuulinda mradi ili kuleta tija inayokusudiwa." Alisema Kheri James
Kwa upande wa Professor Karoli Njau wa Chuo Kikuu Cha Nelson Mandela ambae ni Mshauri mwelekezi wa mradi alisema kuwa wanatumia neti kudaka maji yaliyo kwenye ukungu.Ambapo alizungumza kuwa ukungu una majimaji na unaposhuka chini sana unaweza kutumia teknolojia hiyo iliyowekwa ambayo tunaiona.
"Hii ni teknolojia mpya sana kwa ajili ya kupata maji.Na hii teknolojia ya hizi neti inadaka ule ukungu na ule ukungu unaelekezwa mpaka unafika sehemu za chini ambazo zinakusanya na yale maji yanakusanywa pamoja yanaingizwa kwenye matenki." Alisema Prof. Njau.
Manager wa mradi wa Catching Clouds Dennis Wolter kutoka Ujerumani alisema anashukuru kwa mapokezi makubwa ambayo hakuyategemea, alisema wanakazi kubwa ambayo ipo mbele yao lakini wamejidhatiti na wana shauku kubwa kuifanya.
" Tuna uelewa kwamba tutakutana na changamoto lakini tunavyoona viongozi mnajitoa ni alama kubwa kwamba tunaweza kufanya kazi hii pamoja na tutahakikisha kwa ubora wetu kwamba mradi huu utakuwa wenye tija kubwa kwa jamii.
Kwa upande wa Mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Mbulu Ndugu, Abubakar Kuuli alihitimisha kwa kutoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya watumishi pamoja na wananchi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu, na kueleza kuwa miradi hiyo ni mizuri sana, ule wa kuvuna ukungu na wa kuvuna maji ya mvua. Amewakaribisha wawekezaji na ameahidi kutoa ushirikiano mzuri pale utakapohitajika.
Social Plugin