Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI WA SHAMBA LA MITI SAO HILL WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA UADILIFU


************

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Watumishi wa Shamba la Miti Sao hill Wilayani Mufindi kufanya kazi kwa uadilifu huku akiwataka kutanguliza mbele uzalendo kwa kulinda rasilimali hizo.

Ameyasema hayo jana Agosti 10,2023 alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Shamba hilo katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi za Shamba Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

"Hatutamvumilia mtumishi yeyote anayefanya kazi kwa mazoea" Mhe. Masanja amesisitiza.

Aidha, ameelekeza wahifadhi wa shamba hilo kusimamia vyema maeneo ya misitu yanayovamiwa na wananchi na kuwaondoa wavamizi.

Kuhusu suala la wawekezaji wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu, Mhe. Masanja amesikitishwa na ununuzi wa miti isiyokomaa inayopelekea kutoa bidhaa zisizo la viwango na kuchafua sifa ya Tanzania.

"Tunakataza uvunaji wa miti ambayo haijakomaa.Tuendelee kuhamasisha uwekezaji wa mashamba ya miti ila uvunaji uwe unaokidhi vigezo" Mhe. Masanja amefafanua na kuongeza kuwa Serikali inatamani kushirikiana na wawekezaji kukubaliana juu ya uvunaji wa miti iliyo bora.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja ameitaka Menejimenti ya shamba hilo kushughulikia suala la changamoto ya ukaguzi wa mali zinazoenda bandarini.

"Afisa ukaguzi ahakikishe bidhaa inayoondoka hapa ifanane na inayofika bandarini.Ukaguzi ufanyike vizuri na mzigo ufungwe vizuri" amesema.

Awali, alipokuwa akizungumza na wawekezaji katika viwanda vya uchakataji wa mazao ya misitu kwa nyakati tofauti, Mhe. Masanja aliwaomba wawekezaji hao kuhakikisha wanatumia mazao ya misitu yaliyokomaa ili kuzalisha bidhaa bora.


Ziara ya Naibu Waziri Masanja Mkoani Iringa ni mwendelezo wa ziara zake za kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi na kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com