Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA ASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA SAYANSI NA TEKNOLOJIA



Na.Mwandishi Wetu-MBEYA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekitaka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kuwekeza kwenye Sayansi na Teknolojia ili kuchangia katika kuinuia uchumi.

Prof. Mkenda ametoa rai hiyo wakati akizungumza na Viongozi na Wafanyakazi wa Chuo hicho baada ya kutembelea na kujionea Maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na MUST. Prof. Mkenda ameeleza kuwa kazi ya Chuo Kikuu ni kuzalisha na kusambaza maarifa, kusaka uelewa wa mambo kupitia tafiti, hivyo amesisitiza suala la uwekezaji ili kukiwezesha Chuo hicho kujipambanua vema katika dhana ya kufanya tafiti na gunduzi za Sayansi na kufundisha masomo katika maeneo hayo.

"Tunahitaji kuwekeza lakini katika eneo hili sababu uwezo wetu wa Teknolojia ni duni, nchi yetu na Afrika kwa ujumla zipo nyuma kwenye maeneo ya Sayansi na Teknolojia. Hivyo tunapaswa kuwekeza zaidi ili tuweze kuinua nchi kuwa na teknolohia na zitakazo chochea uchumi" alisema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuwasaidia wataalam na watafiti wanaozalisha maarifa katika sayansi na teknolojia na kuchapisha matokeo ya tafiti hizo katika majarida makubwa duniani, ili kuhamasisha na kuleta ushindani katika nyanja hizo muhimu kwa Maendeleo ya kiuchumi.

Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Prof. Aloys Mvuma amesema kwa kutambua azma ya serikali katika kuboresha Elimu ya Amali, Chuo kimeanzisha Mitaala katika Elimu ya Ufundi, na sasa ina mitaala minne, inayotarajia kutoa Walimu mahiri wenye utaalam wa Uhandisi kwa ajili ya kufundisha Vyuo vya VETA na vile vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs). Prof. Mvuma ameeleza kwamba MUST inajivunia kulea na kuatamia mawazo ya kibunifu yanayovumbuliwa na Wanafunzi, kwani mpaka sasa wanafunzi wanaomaliza hapo wameanzisha kampuni 19 ambazo zimeweza kutoa ajira kwa vijana.

Pamoja na hayo amefafanua kuwa "moja ya mafanikio ni Ubunifu na utengenezaji wa mita za maji za kidijitali, zaidi ya mita 38 zimefungwa sehemu mbalimbali kwa majaribio na matokeo yake ni mazuri" alibainisha Prof. Mvuma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com