Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi mbalimbali kuhusu kuanza kutumika Mitaala mipya ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda,wakati akitoa ufafanuzi mbalimbali kuhusu kuanza kutumika Mitaala mipya ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma
Na.Alex Sonna_DODOMA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Mitaala mipya ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu itaanza kutumika baada ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 kupitishwa na Mamlaka za Maamuzi.
Prof. Mkenda amesema hayo leo Agosti 18 ,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo ameeleza kuwa tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa mitaala hiyo itatangazwa mara baada ya kupitishwa kwa Sera hiyo na kwamba itakapopitishwa utekelezaji utaanza kwa awamu.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa rasimu iliyopo inapendekeza watoto waliopo darasa la Tatu Mwaka huu 2023 ndio watakaosoma mpaka darasa la Sita, hivyo wale waliopo katika madarasa ya Nne, Tano na Sita wataendelea kusoma mpaka darasa la Baba.
"Hatima ya yote utekelezaji huu unategemea mamlaka ya nchi itakaposema tuanze, matumaini yetu ni makubwa kwamba rasimu hii itapita na siku ya kutangazwa kuanza kwa utekelezaji itakuwa ni siku kubwa katika kuelekea mageuzi ya elimu nchini" amesisitiza Prof. Mkenda
Aidha Prof. Mkenda ametoa ufafanuzi kuhusu utaratibu wa Ufadhili wa Samia Skolashipu ambapo amesema Wanafunzi wanaonufaika wasipofikisha GPA 3.8 wataondolewa katika ufadhili huo na kuwekwa kwenye mikopo, lengo ni kuwataka wanafunzi hao kuendelea kusoma kwa bidii na kufanya vizuri.
Amesema kuwa Wanafunzi hao wamesaini mkataba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambao pamoja na mambo mengine unawataka kuhakikisha wana endelea kupata matokeo mazuri na kusomea masomo ya sayansi, Hisabati, Uandisi na Elimu tiba na hawaruhusiwi kubadilisha fani zisizokuwa za Sayansi.
"Ule mkataba unakupa masharti, umeanisha majukumu yako wewe si umefaulu vizuri sana, basi tunatarajia ukienda Chuo Kikuu uendelee kufaulu vizuri, ukishuka tutakuondoa kwenye ufadhili tulakupeleka kwenye mikopo" Alibainisha Prof. Mkenda.
Kuhusu ufundishaji wa somo la dini katika shule za Msingi na Sekondari Prof. Mkenda ameeleza kuwa ukusanyaji wa maoni ya Sera mpya yalihusisha Viongozi wote wa dini kutoka madhehebu mbalimbali ya dini ambao kwa kiwango kikubwa wamechangia katika mapitio ya Sera pia wamehusishwa katika Uandaaji wa mitaala.
"Katika kipindi hiki mageuzi ya Elimu yamekuwa shirikishi, wazi na ya muda mrefu, mwezi Mei mwishoni tulikuwa na Kongamano na lilirishwa mubashara, lilikuwa na Maaskofu, Mashehe, Mapadri Wanazuoni wa dini ya Kiislam na Kikristo walishiriki kwa pamoja". Alieleza Prof. Mkenda
Aidha amesema mitaala inayohusiana na dini inaandikwa na wataalam wa dini wanaoletwa na Taasisi za dini hizo, na kwamba yeyote anaehitaji kuisoma mitaala na mihtasari hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania.
Social Plugin