WILAYA YA BAHI YAJIPANGA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI MAFUNZO YA TEHAMA

Na Dotto Kwilasa,Malunde 1 Blog, Dodoma.

SERIKALI Wilayani Bahi mkoani hapa kupitia Divisheni ya Maendeleo ya Jamii na vijana ina mpango wa kuwawezesha wajasiriamali mafunzo ya TEHAMA ili kuendana na ulimwengu wa kidigitali na kuwasaidia kufanya biashara mtandao na kuwa wa kisasa zaidi.

Hayo yameelezwa leo Agosti 4,2023 Jijini Dodoma na Mkuu wa Divisheni hiyo Denis Komba wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima Nanenane na kueleza kuwa biashara mtandao itasaidia wakulima na wajasiriamali kwa ujumla kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wakati.

Komba amesema tofauti na zamani, mfumo wa uombaji wa mikopo wa sasa unawahitaji wajasiriamali wawe na ujuzi wa kuomba mikopo kwa njia ya mtandao jambo ambalo ni gumu kwao kwa kuwa wengi wao hawana elimu hiyo na kusababisha kuchelewe kupata mikopo kwa wakati na wengine kukata tama ya kukopa Kutokana na usumbufu wanaoupata.

"Wajasiriamali wengi tunao wahudumia hawajui matumizi ya TEHAMA,wengi ni wa pembezoni,Dunia inatutaka tuendane na teknolojia hii hivyo kwa kuanza tumeanza kuwaelimisha Maafisa Kata kwenye Kata tano Bahi ili waweze kuwasaidia wajasiriamali kujisajili kwa ajili ya mikopo na baadae tutawafikia wajasiriamali wote ,"amefafanua 

Amefafanua kuwa ili kufanikiwa kwenye masuala ya uwekezaji na masoko, Wilaya ya Bahi imejipanga kuwanufaisha vijana, wanawake na wenye ulemavu kulima Kilimo biashara na kuongeza thamani ya mazao na hivyo kupitia teknolojia hiyo itasaidia Ubunifu na tija.

Komba amesema kupitia maonyesho ya wakulima yanayoendelea Jijini hapa,Ofisi yake imefanya jitihada za kuyafikia makundi hayo na kuwaelimisha namna bora ya kulima kwa tija na kuzifanya za Kilimo kuwa biashara na hatimaye kupelekea kuwa ajira.

"Tunawatengeneza vijana na Jamii Kwa ujumla kupitia biashara zao kupata ajira,tunataka Kila mmoja aone thamani ya Kilimo biashara kuwa ni ajira,kupitia hamasa tunayoitoa watu wataachana na kilimo cha zamani na kuanza kubadilika,"amesema

Pamoja na hayo amesema ili kuwezesha vijana kufanikiwa zaidi,Ofisi hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya riba Nafuu Kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu wa Wilaya hiyo ili kuwasaidia lijikwamua kiuchumi.

"Tunaendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia vikundi vyao kwa kuwakopesha, Dunia ya Sasa inahitaji  bidhaa zenye thamani ya Ubunifu na ubora ili soko la uhakika liwepo,kwa kuliona hili tayari kwa mwaka wa fedha 2022/2023 tumewawezesha watu 123 lengo ni kuwafikia watu 150,"amefafanua Komba

Mkuu huyo wa Divisheni ya maendeleo ya jamii ametumia nafasi hiyo pia kuwahamasisha vijana kuendelea kushiriki maonesho hayo kujifunza mbinu Mpya za uzalishaji  ili kuboresha mazingira ya kilimo Kanda ya kati na hatimaye Tanzania Kwa ujumla.

Naye Afisa Kilimo,Uvuvi na Mifugo Wilaya ya Bahi Siwajibu Seleman ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wawekezaji wa Viwanda nchini kuwekeza Wilayani humo ili kuongeza ari ya wakulima kuzalisha zaidi na kuleta tija ya thamani ya mazao na kusema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuwainua wakulima .

Amesema uwepo wa Viwanda Bahi utaongeza uhakika wa wakulima kulima mazao mengi na kuwa na soko la uhakika na kuondokana na hofu ya kuharibika kwa mazao yao .

"Kuna wakati wakulima wanatamani kulima zaidi lakini wanahofu kupoteza nguvu zao,njia pekee ya kuwaokoa ni kuwepo Viwanda vya usindikaji hali itakayo wainua kiuchumi na kuwa na maisha bora,"amesema

Ametaja baadhi ya maeneo ya uwekezaji kwenye Wilaya hiyo kuwa ni Ufugaji wa Ng'ombe,uvuvi,Kilimo cha mpunga, Alizeti,zabibu,mtama Pamoja na Kilimo cha mahindi.

Amesema zao la alizeti  kwenye Wilaya hiyo ni la kimkakati na hivyo kupewa kipaumbele katika kuchochea biashara na uwekezaji huku zao la mtama likitiliwa mkazo kwa ajili ya chakula.

"Asilimia 70 ya wakazi wa Bahi wanajihusisha na kilimo pamoja na ufugaji,tunajivunia kuwa na Mifugo mingi kulingana na mahitaji ambapo kuna Ng'ombe zaidi ya laki tatu pamoja na mbuzi zaidi ya laki moja na nusu,"amesema





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post