Afrika Kusini na Marekani zitaanza majaribio ya chanjo mpya ya kuzuia VVU na zimeanza kuwaandikisha washiriki kushiriki katika majaribio ya kimatibabu.
Kulingana na shirika la utafiti la serikali la Marekani la Taasisi za Kitaifa za Afya (NIH), chanjo hiyo, iitwayo VIR-1388, imeundwa kusaidia seli za T za mwili, zinazosaidia mfumo wa kinga kupambana na vijidudu na kukinga dhidi ya magonjwa.
Chanjo hiyo inakusudiwa kuelekeza mfumo wa kinga ya mwili kuzalisha T-seli "zinazoweza kutambua VVU na kuashiria mwitikio wa kinga ili kuzuia virusi kuanzisha maambukizi ya muda mrefu".
Jaribio la chanjo hiyo linafadhiliwa na NIH, Wakfu wa Bill na Melinda Gates na kampuni ya Marekani ya Vir Biotechnology.
Utafiti huo utaandikisha washiriki 95 wasio na VVU katika maeneo manne nchini Afrika Kusini na maeneo sita nchini Marekani.
Matokeo ya awali ya jaribio la chanjo yatatangazwa mwishoni mwa 2024, lakini baadhi ya washiriki wataendelea na majaribio kwa miaka mitatu.
Mnamo mwaka wa 2020, NIH ilisitisha majaribio ya chanjo nyingine ya VVU nchini Afrika Kusini baada ya ukaguzi kugundua kuwa chanjo hiyo haikuwa na ufanisi katika kuzuia maambukizi ya VVU.
CHANZO- BBC SWAHILI
Social Plugin