Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CUHAS YAZINDUA MBIO ZA HISANI KUWACHANGIA ADA WANAFUNZI WASIOJIWEZA

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga (Wa pili Kulia) akikimbia mbio za hisani zinazolenga kuchangisha fedha za Ada kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma katika Mbio za hisani kichangia ada za wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za afya na Tiba Shirikishi (CUHAS). Wengine ni Mbunge wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula (wa tatu kulia), na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo CUHAS, Profesa Peter Lambau (wa nne kulia). Picha na Mgongo Kaitira.

****
Wanafunzi 152 wanaosoma fani mbalimbali ngazi ya Stashahada na Shahada katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Sayansi za afya na Tiba Shirikishi (CUHAS) wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kumudu gharama ya Ada.


Kutokana na changamoto hizo, Cuhas imeanzisha Mbio za Hisani zenye lengo la kuchangisha fedha angalau kuanzia Sh50 milioni ambazo zitatumika kugharamia Ada za wanafunzi hao ili watimize lengo la kupata elimu sambamba na kuongeza idadi ya wataalam katika Sekta hiyo.


Uzinduzi wa mbio hizo umefanyika leo na kushuhudiwa na mamia ya watumishi wa Bugando, Cuhas, wanafunzi na wadau wa Taasisi hizo huku Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Cuhas (Cuhasso), Deus Charles akisema mbio hizo ni jitihada zinazofanyika ili kunusuru wanafunzi wanaosoma fani ya Udaktari, Ufamasia, Uuguzi, Wataalam wa Maabara na Mionzi ambao wako hatarini kusitisha masomo yao kwa changamoto hiyo.


Charles amesema fedha hiyo itakayohifadhiwa katika Mfuko Maalum wa Kufadhiri Wanafunzi wenye changamoto ya ada (Cuhas Education Fund) itaanza kwa kugharamia wanafunzi hao kuanzia mwaka huu.


Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Fabian Massaga amesema hospitali hiyo inatarajia kuanzisha mbio za hisani (Bugando Marathon) zenye lengo la kuchangisha fedha za kugharamia matibabu ya wagonjwa wanaoshindwa kumudu gharama hospitalini hapo.


"Tunaungana na CUHAS kufanikisha uchangishaji wa fedha hizi ili tufanikishe malipo ya ada kwa wanafunzi wanaoshindwa kumudu gharama za elimu chuoni hapo. Lengo ni kuhakikisha tunatengeneza watalaam wa kutosha katika sekta ya afya nchini," amesema
"Jumuiya ya Bugando kwa kuonyesha mfano kwa jamii tunayoihudumia tayari tumetenga siku ya Jumanne na Ijumaa asubuhi kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo ambayo yanasaidia kuimarisha vifo na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambapo sasa yamekuwa tishio kwa wananchi wengi," ameongeza

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Cuhas, Profesa Peter Lambau amesema fedha hiyo itatumika kugharamia ada ya wanafunzi zaidi ya 152 wanaosoma Shahada na Stashahada za fani mbalimbali wenye changamoto ya kukosa ada chuoni hapo.

Tumekuwa tukipoteza wataalam katika fani za afya na wengi wao wanashindwa kumudu gharama ya ada. Tunatambua kwamba Serikali inatoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya Elimu ya Juu na kati lakini tumeona turahisishe kumaliza changamoto kwa wasilipiwa fedha yote," amesema Profesa Lambau.

Kutokana na kuanzishwa kwa mbio hizo, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula amechangia Sh6 milioni kutoka katika mfuko wa jimbo huku akiahidi kuendelea kuhamasisha wadau wengine kujitokeza kuchangia ada ili kufanikisha masomo kwa wanafunzi hao.

Mabula amesema pamoja na juhudi za Serikali kuwekeza nguvu kubwa kwenye utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati na juu, bado jitihada zinahitajika kuhakikisha kila mwanafunzi anafikia malengo yake ya kupata elimu nchini bila kujali hali yake ya kipato.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com