*Mkurugenzi Mkuu amueleza Naibu Waziri Mkuu jinsi wanavyowafikia wachimbaji wadogo
*Mkoa wa Geita pekee walikusanya bilioni 56 kwa mwaka fedha ulioishia Juni 2023
Na MWANDISHI WETU, GEITA
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amemueleza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kuwa NSSF inashiriki Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini kwa sababu ndio Mfuko pekee wenye jukumu la kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na baadaye.
Mshomba amesema hayo tarehe 23 Septemba, 2023 alipokuwa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mkuu alipotembelea banda la NSSF katika maonesho hayo yenye kauli mbiu isemayo ‘Matumizi ya Teknolojia Sahihi katika Kuinua Wachimbaji Wadogo Kiuchumi na Kuhifadhi Mazingira’ yanayoendelea katika viwanja vya EPZA, Bombambili Mkoani Geita.
Amesema tokea maonesho hayo yalipoanza mwaka 2018, NSSF imekuwa na mafanikio makubwa kwani ushiriki wake umechangia ukuaji wa Mfuko ambapo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023, walikusanya michango ya takribani shilingi bilioni 56.
“Wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, hapa Mkoani Geita pekee NSSF ilikuwa inakusanya michango ya shilingi bilioni 29 ambayo ni mara mbili katika kipindi hiki cha miaka miwili na nusu ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, kwa hiyo kwetu sisi ni mafanikio makubwa sana na tunaamini tutaendelea kufanya vizuri zaidi,” ameeleza Mshomba.
Aidha, amesema mafanikio ya NSSF kwa ujumla ni mazuri ambapo katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2023, thamani ya michango iliyokusanywa ilikuwa ni ya shilingi trilioni 1.66 na katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2022, thamani ya michango iliyokusanywa ilikuwa ni shilingi trilioni 1.48.
Mshomba amesema hilo ni ongezeko kubwa na kwamba thamani ya NSSF imeendelea kukua kwa kasi ambapo kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa mwezi Juni 2022, thamani ya Mfuko ilikuwa trilioni 6.08 na kuwa mpaka kufikia mwezi Juni 2023 thamani ya Mfuko imefikia trilioni 7.6 kwa hesabu ambazo zinaendelea kukaguliwa.
“Huo ni ukuaji mkubwa mno hasa ukizingatia kabla ya hapo na baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani thamani ya Mfuko ilikuwa ni trilioni 4.8 hivyo mafanikio hayo ni kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais ya kuvutia wawekezaji,” amesema Mshomba.
Amesisitiza kuwa, maonesho hayo ya madini tokea yalipoanza yamekuwa chachu ya ongezeko hilo la wanachama na michango, ambapo ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Geita chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Martine Shigela kwa ushirikiano mkubwa wanaowapatia.
Kuhusu matumizi ya TEHAMA, Mshomba amesema NSSF imeweka kipaumbele kikubwa katika matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha huduma za wanachama wao jambo ambalo linaendana na kauli mbiu ya maonesho ya madini.
Mshomba amesema NSSF inaendelea kusajili wanachama wapya kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi hususan wachimbaji wadogo ambao ndio lengo la Mfuko kushiriki katika maonesho hayo ya madini.
Social Plugin