Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI SHINYANGA WANASA NOTI BANDIA, SILAHA, WAGANGA WA KIENYEJI, PIKIPIKI ZILIZOBEBA MIZIGO HATARISHI BARABARANI




Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watuhumiwa 12 na wengine limewafikisha mahakamani kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kukamatwa noti bandia 15 zenye thamani ya Tsh, 150,000/=, silaha, wizi na kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali wakiwa na vifaa vya ramli chonganishi.


Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamisi Septemba 21,2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema watuhumiwa hao wamekatwa kupitia misako na doria iliyofanywa katika maeneo mbalimbali katika kipindi cha mwezi Agosti mpaka Septemba, 2023 ikiwa ni katika kuendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda maisha ya watu na mali zao.


“Katika muendelezo wa misako hiyo tuliweza kukamata noti bandia 15 zenye thamani ya Tsh, 150,000/=, dawa za kulevya aina ya Bangi yenye uzito wa Kg. 40 na kete 18, Heroine kete 01, Pikipiki 16 zilizokuwa zikitumika katika kutendea makosa mbalimbali, mashine 01 ya kufua umeme, mashine 01 ya kuchomelea vyuma, lita 120 za mafuta ya kuendeshea mitambo, pamoja na vipande 880 vya nondo”,ameeleza Kamanda Magomi.
“Lakini pia katika misako hiyo tulifanikiwa kuwakamata waganga 03 wa kienyeji kwa kufanya shughuli za uganga bila kibali na pia wakiwa na vifaa mbalimbali vya ramli chonganishi, Sub-woofer 01, TV 01, viti 20, pamoja na lita 76 za pombe ya moshi”,ameongeza.

Amefafanua kuwa pia wamefanikiwa kukamata Silaha aina ya Shortgun BELGIUM yenye namba 18342 ambayo ilikuwa inamilikiwa isivyo halali.

"Pia tumekamata silaha nyingine aina ya Shortgun Pump Action yenye namba za usajili TZ CAR 69657A ambayo ilitumika katika tukio la unyang'anyi na kuitelekeza baada ya kugundua kuwa wanafuatiliwa na askari", ameongeza.


“Jumla ya watuhumiwa 12 wanashikiliwa kuhusiana na makosa hayo na wengine wameshafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria huku wengine wakipewa dhamana huku wakisubiri Upelelezi kukamilika”,ameeleza.


Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, amesema Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita lilifanikiwa kukamata jumla ya makosa mbalimbali 3636 ya usalama barabarani ambapo jumla ya magari yaliyokamatwa yalikuwa 2850. Magari mabovu ni 1053, kuzidisha abiria ni 429, kutokuwa na Bima ni 163, kuendesha magari kwa njia hatarishi ni 139, kutofunga mikanda ya usalama ni 31, kuendesha magari bila leseni ni 05 na kuendesha magari kwa mwendokasi ni 509, makosa mengineyo 521.
“Pia jumla ya Pikipiki na Bajaji 786 zilikamatwa kwa makosa mbalimbali ambapo Pikipiki mbovu zilikuwa ni 59, kutovaa kofia ngumu ni 182, kuzidisha abiria ni 76, kuendesha Pikipiki bila Bima ni 163, kuendesha pikipiki kwa njia hatarishi ni 33, kulewa na kuendesha pikipiki ni 01, kuendeha pikipiki bila leseni ni 203 na kutokuwa na leseni ya usafirishaji ni 69”,amesema.


Akielezea mafanikio yaliyofikiwa na Jeshi la Polisi katika kipindi cha Mwezi Agosti hadi Septemba 2023, Kamanda Magomi amesema mtuhumiwa 01 wa kesi ya kubaka alihukumiwa kifungo cha maisha jela na watuhumiwa wengine 04 walihukumiwa kifungo cha miaka 30 Jela kila mmoja kwa kosa hilo hilo la kubaka ambapo walitenda makosa hayo katika nyakati tofauti.


“Katika kipindi hicho, kesi za wizi zilikuwa 03 na zilihukumiwa kulipa faini kati ya Tsh. 100,000/= hadi 500,000/=, kesi 01 ya kutelekeza familia mshtakiwa alifungwa miezi 06 jela, kesi 01 ya kutorosha mwanafunzi ilihukumiwa kuchapwa viboko 05, kutupa mtoto kesi 01 ilihukumiwa miaka 02 kutumikia jamii, kupatikana na Bangi kesi 01 ilihukumiwa kutumikia jamii mwa kipindi cha mwezi 01 na pia kupatikana na madawa ya kulevya kesi 02 zilihukumiwa kifungo cha miaka 02 jela”,amesema.

Kamanda huyo wa Polisi amesema Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linaendelea kuwashukuru raia wema wote wanaotoa taarifa za uhalifu na wahalifu zinazoleta mafanikio haya na linawaasa wananchi wote kuendelea kutii sheria za nchi kuuweka mkoa wa Shinyanga kwenye ushwari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Septemba 21,2023.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamis Septemba 21,2023.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha silaha na vitu mbalimbali vilivyokamatwa na Polisi Shinyanga
Vitu mbalimbali vilivyokamatwa na Polisi Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi vitu mbalimbali vilivyokamatwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha bangi iliyokamatwa na Polisi Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha pikipiki zilizokamatwa kwa kubeba mizigo hatarishi barabarani
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha vitu mbalimbali vilivyokamatwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionesha viti vilivyokamatwa
Nondo zilizokamatwa na Polisi Shinyanga
Vitu mbalimbali vilivyokamatwa na Polisi Shinyanga
Pikipiki zilizokamatwa na Polisi Shinyanga

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com