Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Simiyu, imeanzisha mradi wa kiuchumi, lengo likiwa kuimarisha uwezo wake wa kujiendesha bila ya kutegemea wafadhili wa ndani na nje ya nchi.
Mradi huo ni Pikipiki Mbili aina ya SANLG, uliogharimu zaidi ya Milioni 5, ambapo Klabu hiyo imeweza kuajili vijana wawili kwa ajili ya kufanyia Biashara ya kusafirisha abiria (BodaBoda).
Akiwakabishi Pikipiki hizo, Mwenyekiti Kamati ya Uchumi na Fedha SMPC Bw. Sitta Tuma amewataka vijana hao kuhakikisha Pikipiki hizo wanazitunza na kuziona kama mali yao.
" Hizi Pikipiki tumewapatia Leo, zitunzeni ili ziweze kukaa kwa muda mrefu, hakikisheni pia mnazingatia sheria zote za Usalama Barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu kila wakati", amesema Bw. Tumma.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Simiyu (SMPC) Frank Kasamwa, amesema kuwa mradi huo unakwenda kupunguza suala la utegemezi kwa Klabu hiyo.
SMPC imeingia Mkataba wa Mwaka mmoja kwa kila kijana aliyepatiwa Pikipiki, ambapo baada ya Mkataba kuisha Pikipiki hizo zitakuwa Mali ya vijana hao.