Afisa Biashara kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Nchini Bw. Marcel Kasongo Yampanya amewasilisha nia ya Serikali ya Kongo kuleta Vijana wengi nchini Tanzania kujifunza Uongezaji Thamani wa Madini ya Vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha jijini Arusha.
Ameyabainisha hayo wakati wa mazungumzo yake na viongozi wa kituo cha TGC baada ya kukitembelea Septemba 19, 2023 katika ziara iliyolenga kujifunza na kuona namna ya kushirikiana na kituo hicho katika masuala ya Uongezaji Thamani Madini ya Vito pamoja na kuhakikisha ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili katika kukuza sekta hiyo ndogo.
Ziara hiyo inakuja wakati ambapo nchi ya Kongo imeonyesha nia ya kukuza sekta ya madini ya vito na kuleta vijana wa Kongo kujifunza kutoka kwa wataalam wa Tanzania ambao wamekuwa wakiongoza katika utoaji wa mafunzo ya uongezaji thamani wa madini ya vito kwa upande wa Afrika ya Mashariki na Kati.
Aidha, sehemu kubwa ya wakufunzi wa kituo hicho tayari wamepata utaalam wa shughuli hizo kutoka nchi mbalimbali zilizoendelea katika eneo hilo ikiwemo Thailand, India na China.
Aidha, ziara hiyo ya Afisa biashara wa Kongo imekuja ikiwa zimepita siku chache tu baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea shughuli za uongezaji thamani madini katika viwanda vikubwa, vya kati na vidogo nchini Thailand ambapo shughuli hizo zimeshamiri kwa kiasi kikubwa. Katika ziara hiyo, Mratibu wa Kituo hicho pia alikuwa sehemu ya ujumbe huo.
Katika ziara ya hivi karibuni nchini Thailand, Wizara ya Madini kupitia kituo hicho ilifanya mazungumzo na taasisi kadhaa kuhusu namna ya kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uongezaji thamani ikiwemo kiwanda kikubwa chenye uzoefu wa miaka 50 katika shughuli za uongezaji thamani madini ambapo wadau nchini humo walifungua milango kwa watanzania kujifunza ili kuwa bora katika eneo hilo.
Katika kikao hicho, Kaimu Mratibu wa TGC Bw. Daniel Kidesheni amepokea ahadi ya balozi na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya taasisi hizo mbili. Amesisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na kuendeleza teknolojia za kisasa ili kuhakikisha kuwa sekta ndogo ya madini ya vito inachangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo katika nchi hizo.
Katika ziara hiyo, Bw. Kasongo amepata fursa ya kutembelea karakana mbalimbali za TGC, ikiwa ni pamoja na maabara za kisasa zinazotumika kwa uchunguzi wa madini ya vito, usonara na ukuataji na ung’arishaji wa madini ya Vito.
Ziara hiyo ya Afisa biashara kutoka ubalozi wa Kongo nchini Tanzania imekuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ndogo ya madini ya vito.