Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi Mhe David Kihenzile ameridhishwa na utekelezwaji wa mikakati ya ufundishaji katika Chuo cha taifa cha usafirishaji na mipango ya uendeshaji wa reli ya TAZARA na kuwataka kubuni zaidi ili kuongeza mapato.
Mhe Kihenzile ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea, kujifunza, kujitambulisha na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na TAZARA ikiwemo Karakana ya ukarabati wa mabehewa na vichwa vya treni na miradi ya ujenzi,karakana ya matengenezo ya ndege na simulator ya ndege vilivyopo Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Jijini Dar es salaam tarehe 29 Septemba,2023
“ Shirika la TAZARA na Chuo cha NIT ni muhimu sana kwa maslahi ya Taifa letu, wataalamu wa usafiri na usafirishaji wengi wa ndani na nje ya nchi wanapita hapo na mizigo inayoelekea Zambia na kipande kizima cha ukanda wa SADC inabebwa na reli ya TAZARA, hivi ni muhimu sana kwa uchumi wetu” amesisitiza kihenzile
Mhe kihenzile amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanya maboresho makubwa kwenye sekta ya uchukuzi hivyo itahitaji wataalamu zaidi kwa uendeshaji na kuwataka NIT kujipanga vyema zaidi vilevile maboresho ya bandari zetu za bahari, maziwa sambamba na ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo vitaongeza mzigo zaidi unaohitaji kuhudumiwa nchini hivyo maboresho makubwa yatafanywa kwenye reli ya TAZARA ili kuiongezea uwezo wa bubeba mizigo zaidi na kuwataka kubuni zaidi ili kuongeza mapato.
“TAZARA ilitengenezwa na uwezo wa kubeba mzigo wa metric tani mil 5 kwa mwaka lakini mpaka sasa inabeba tani 240,000 kutokana na mipango ya maboresho makubwa yatakayoanza kufanywa na Serikali kwenye reli hii yataiwezesha kubeba mzigo wa metric tani mil 30 kwa mwaka pia utaratibu unaofanyika wa kuruhusu wawekezaji binafsi(open access) vitaleta ushindani zaidi na kuongeza tija kwa Taifa na tayari ndege mbili zimeshafika kwa ajiri ya NIT anzeni kuongeza ubunifu kibiashara” amesisitiza Kihenzile
Akimkaribisha Naibu Waziri Mkurugenzi mkuu wa TAZARA,Mha Bruno Ching’andu amesema njia ya Tazara ina urefu wa kilomita 1,860 na kwa sasa Shirika lina vichwa vya treni 12 ambapo vichwa 4 vimetegwa kwa ajili ya abiria,3 mizigo na 1 kwa uhandisi na mabehewa 400 likiwa na uwezo wa kuhudumia mzigo wa tani 240,000 kwa mwaka pamoja na kuwepo kwa changamoto za upungufu wa rasilimali fedha,wataalam na uharibifu wa miundombinu.
Akitoa maelezo ya miradi Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof Zacharia Mganilwa ameishukuru Wizara ya Uchukuzi na Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi ujenzi na uboreshwaji wa miundombinu ya kufundishia na malazi chuoni hapo hali iliyoongeza udahili kutoka wanafunzi 6,000 mwaka 2020 mpaka elfu kumi na tano mwaka 2023.
Social Plugin