Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KISHAPU YAADHIMISHA SIKU YA USAFISHAJI DUNIANI

Na Sumai Salum - Kishapu
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imeadhimisha siku ya Usafishaji Duniani "World Cleanup Day" katika soko la Mhunze, mitaro ya barabara ya Kishapu-Meatu na barabara ya ndani.

Maadhimisho hayo yamefanyika leo Septemba 16,2023  yakihusisha watumishi wa idara ya afya na mazingira, jeshi la polisi ,watendaji wa kata na kijiji,wafanyabiashara,wajasiriamali,wananchi pamoja na wanafunzi wa kidato cha tano shule ya Sekondari Kishapu.

Akizungumza baada ya usafi ulioanza saa 1 hadi saa 4 asubuhi Robert Paul mwanafunzi wa kidato cha tano shule ya Sekondari Kishapu amesema utunzaji mazingira inatakiwa kuwa tabia ya kila mtu endapo mazingira yakiwa safi wataepukana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

Kwa upande wake Charles Faustine (mwanafunzi) amesema kuwa anajisikia fahari kuwa miongoni mwa washiriki wa usafi wa mazingira kwani mazingira yakiwa safi yanavutia hata uwekezaji.

Mwenyekiti wa Kishapu Veteran Sostenas Amasi amesema wao kama mabalozi wa mazingira wana jukumu la kuendelea kuihamasisha jamii kuendelea kutunza mazingira kwa kufanya usafi na kuweka taka mahali panapohitajika.

Hata hivyo afisa afya wa kata ya Kishapu, Keneth Faustine amekiri kuwa kwa sasa wananchi wa Kishapu wamekuwa na mwitikio mzuri wa kushiriki masuala ya utunzaji mazingira tofauti na hapo awali jambo lililopelekea usimamizi wa zoezi hilo kutokuwa gumu.

"Kiukweli Kishapu ya sasa sio ile ya miaka 10 au 5 nyuma hata tulipotangaza biashara zitafunguliwa saa 4 asubuhi tunaona watu wametii na kufanya usafi japokuwa wapo baadhi yao wachache ambao bado hawana mwitikio hivyo tutaendelea kutoa elimu zaidi kadri tunavyoendelea na tunaamini watabadilika na Kishapu itakuwa ni mji wa kuvutia kabisa",amesema Faustine.

Sambamba na hayo afisa mazingira wa halmashauri hiyo, Charles Kanwakabo amesema zoezi Hilo lipo kwa mujibu wa Sheria na mkataba wa kutoka shirika la mazingira duniani kuwa kila mwaka ifikapo Septemba 16 watu wote washiriki zoezi la pamoja la Usafi.

"Nipende kutoa wito kwa jamii hasa ya wafanyabiashara kuwa sehemu iliyo safi inavutia wateja,mteja haji sehemu chafu kununua bidhaa,lakini pia uwe ni utaratibu wetu wa kila siku kufanya usafi kuanzia vyooni hadi nje ya maeneo yetu lakini pia usafi wetu binafsi kwani mtu akiwa safi anakuwa naujasiri ndani yake",amesema Kanwakabo

Septemba 16 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya Usafishaji" World Cleanup Day" yenye maana ya kukabiliana na uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
Wanafunzi wakiendelea kufanya usafi
Wanafunzi wakiendelea kufanya usafi
Afisa mazingira wa halmashauri ya Kishapu, Charles Kanwakabo
Afisa afya wa kata ya Kishapu, Keneth Faustine

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com