Usalama wa chakula ni jukumu la kila mtu. Unaanzia shambani, hadi nyumbani ambapo mazao yanatumika, yaani kwa mlaji. Afya ya mwanadamu inategemea chakula bora na salama. Kama hakitakuwa salama, chakula hicho humletea madhara, na pengine hata kifo.
Ili kuepukana na athari hizo, kila mtu popote alipo anaweza kusaidia kupunguza vihatarishi vya afya ya wanadamu vitokanavyo na chakula kutokuwa salama.
Zipo faida nyingi za ulaji wa chakula salama. Unapokula chakula salama unaepuka magonjwa, mwili unakuwa na afya nzuri, gharama za matibabu zinapungua na humfanya mtu afanye kazi zake vizuri na kuishi maisha marefu.
Suala la usalama wa chakula siyo tu katika familia; ni la kitaifa, kikanda na kimataifa. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango, alipokuwa katika kongamano la Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika mwaka 2022, lililofanyika Kigali, Rwanda, lililohusisha wakuu wa nchi na serikali, alisema hivi “Agenda ya usalama wa chakula inapaswa kuendelea kujadiliwa katika mijadala mingine, ikiwezekana ya kikanda na ya Umoja wa Nchi za Afrika kwa sababu inagusa maisha ya kila siku”.
Alisema hayo wakati wakuu hao walipokuwa wakijadili namna nchi za Afrika zinavyoweza kukabiliana na tishio la usalama wa chakula.
Alisema kuwa Serikali ya Tanzania inafanya jitihada za kuinua sekta ya kilimo, ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta hiyo, ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula barani Afrika.
Ni dhahiri kabisa kuwa usalama wa chakula ni usalama wa mtu, familia na nchi kwa ujumla. Ukiona viongozi wa nchi wanaacha yaliyoko nchini mwao wanakuja Tanzania kujadili usalama wa chakula wa bara zima la Afrika, tambua kuwa chakula ni chanzo cha uhai wa mwanadamu na ustawi wake.
Hapa tutaona hatua ambazo serikali imekuwa ikichukuwa kuhakikisha kuwa usalama wa chakula unapewa kipaumbele katika taifa letu, ili ujue jitihada ambazo serikali imekuwa ikichukuwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula,
Leo nitaongelea Idara ya Usalama wa Chakula ilivyoanza na majukumu yake ni nini. Wale wa umri wa miaka arobaini na kuendelea, mtajikumbusha kuhusu maduka ya NMC na ugawaji wa chakula; nayo yalikuwa ni kuhakikisha watu wanapata chakula. Fuatana nami.
Serikali kwa nyakati zote tangu tupate Uhuru imefanya jitihada katika sekta ya kilimo kwa kuweka mifumo na kutumia mikakati mbalimbali kuhakikisha Taifa linajitosheleza kwa chakula. Sheria ya Mazao (Agricultural Produce Act 1962) na ile ya Food Security Assistance Scheme ya mwaka 1976, zote zililenga katika kupunguza uagizaji wa chakula kutoka nje ya nchi. Matokeo yake yalikuwa ni uanzishaji wa Ghala la Taifa la Nafaka (SGR), chini ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), pamoja na uundaji wa Kitengo cha Uratibu wa Mazao na Tahadhari ya Njaa (Crop Monitoring and Early Warning Unit) kilichokuwa chini ya Wizara ya Kilimo.
Mwaka 1986, vipengele mbalimbali vilivyosabababisha uhaba wa chakula vilitambuliwa na hatua za kuvirekebisha pia ziliainishwa. Hii ni pamoja na Sheria ya Usalama wa Chakula (The Food Security Act). Sheria hiyo iliondoa shughuli mbalimbali zinazohusiana na mazao ya chakula kutoka Shirika la Usagishaji la Taifa kwenda Wizara ya Kilimo na Chakula, chini ya Idara ya Usalama wa Chakula.
Mwaka 1994, ulianzishwa Mkakati wa Taifa wa Chakula, ambao ulilenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuboresha hali ya lishe ya watu walio katika makundi hatarishi.
Aidha, mwaka 1995, Programu Maalum ya Taifa ya Usalama wa Chakula ilianzishwa chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO). Programu ililenga kuongeza uzalishaji wa mazao makuu ya chakula kwa kuboresha huduma za ugani, kwa utaratibu wa kupitia vikundi maalum vya wakulima vilivyoteuliwa kama maeneo ya mfano. Kiuhalisia, Programu ilifanikiwa. Mafanikio hayo yalienezwa na kutumika katika maeneo mbalimbali nchini., Idara ya Usalama wa Chakula chini ya Wizara ya Kilimo na Chakula,. Majukumu yake makubwa yalikuwa kama ifuatavyo:
(i) Kubuni sera, kuandaa mikakati na kuratibu utekelezaji wa programu za usalama wa chakula
(ii) Kuratibu hali ya chakula nchini na kutoa tahadhari ya njaa
(iii) Kufanya tathmini za kisera kuhusu usalama wa chakula
(iv) Kuhifadhi mazao kwa lengo la kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno
(v) Kuhamasisha matumizi ya mazao mbalimbali ya chakula kwa lengo la kupanua wigo wa aina ya vyakula vikuu vinavyotumiwa na jamii
(vi) Kuhamasisha usindikaji wa mazao ya chakula katika maeneo ya uzalishaji kwa lengo la kuongeza ubora, muda na eneo la matumizi
(vii)Kuhamasisha usindikaji ili kuongezea mazao thamani
Chimbuko la uanzishwaji wa akiba ya chakula ya Taifa lilitokana na ukame ulioikumba nchi yetu miaka ya 1973 hadi 1975 na kusababisha baa kubwa la njaa, hali ambayo ilifanya nchi kutegemea chakula kutoka nje ya nchi, kilichoagizwa pamoja na chakula cha msaada kutoka kwa nchi wahisani. Baada ya baa hilo la njaa, Serikali iliamua kubuni mkakati pamoja na kuanzisha chombo mahsusi kinachomilikiwa na Serikali, ambacho kilipewa jukumu la kununua na kuhifadhi chakula cha akiba. Chombo cha kwanza kuundwa kwa madhumuni hayo ni Bodi ya Mazao ya Kilimo (National Agricultural Produce Board–NAPB) mwaka 1973, na baadaye likaanzishwa Shirika la Usagishaji la Taifa (National Milling Corporation–NMC).
Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) lilikuwa na majukumu makuu mawili, ambayo ni kuendesha biashara ya chakula (commercial role), na kusambaza chakula kwa waathirika na njaa (social role). Katika miaka ya 1990, Serikali ilichukuwa hatua ya kuondoa SGR kutoka NMC, na kuwekwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo. Mwaka 1990/1991, SGR ilikuwa na kiasi cha tani 107,000 za mahindi kwa ajili ya akiba ya chakula ya Taifa. Shughuli za SGR zimeendelea kuimarishwa, ambapo mwaka 2008 ulianzishwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (National Food Reserve Agency–NFRA). NFRA inafanya kazi katika kanda saba, ambazo ni Arusha, Dodoma, Kipawa, Makambako, Shinyanga, Songea na Sumbawanga. NFRA kwa sasa ina maghala ya kuhifadht nafaka na imejipanga kununua nafaka kutoka kwa wakulima, kuhifadhi na kutumia pale inapohitajika.
Lakini ikumbukwe kuwa usalama wa chakula ni suala la kila mtu. Je, wewe mchango wako uko wapi katika hili, unalima, ndiyo. Je, unazuiaje chakula hicho kisipotee. Umenunua sokoni chakula kikiwa bora na salama, unakiandaaje, unakitunzaje na unakitumia vipi ili kikiisha kisilete madhara kwa mlaji na wewe unaye kiuza unakitunza vipi na kwa muda gani?
Usalama wa chakula unatuhusu wote mtu mmoja mmoja, familia, jamii na taifa. Hakuna taifa lenye njaa duniani, ambalo liko salama na watu wake wametulia. Suala la usalama wa chakula tunaliona tangu enzi za Farao, wakati wa Yusufu hadi leo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.