Zoleka Mandela, mjukuu wa Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini Nelson Mandela, amefariki dunia kwa saratani akiwa na umri wa miaka 43, familia yake imetangaza.
Katika taarifa kwenye Instagram, msemaji alisema kuwa Zoleka aliaga dunia Jumatatu jioni akiwa amezungukwa na marafiki na familia.
Katika miaka ya hivi majuzi alijulikana sana kwa kuelezea matibabu yake ya saratani na pia kuwa wazi juu ya historia yake ya uraibu wa dawa za kulevya na mfadhaiko, na ukweli kwamba alidhulumiwa kingono akiwa mtoto.Aliandika hadithi yake katika tawasifu When Hope Whispers.
Zaidi ya muongo mmoja uliopita Zoleka alikuwa amegundulika kuwa na saratani ya matiti, alipata matibabu na alikuwa katika hali ya utulivu lakini baadaye ikarejea.
Mwaka jana, alithibitisha kuwa alikuwa na saratani kwenye ini na mapafu, kisha ikasambaa kwa viungo vingine.
Alikuwa akipokea matibabu na kulazwa hospitalini tarehe 18 Septemba."Nilifanyiwa uchunguzi wa CT scan wiki chache zilizopita, ambayo imeonyesha kuwa nina damu iliyoganda pamoja na uvimbe wa Fibrosis kwenye pafu langu. Hii inaelezea maumivu ya kifua niliyokuwa nikiyasikia.
Daktari wangu wa saratani amependekeza dawa za kupunguza damu na tiba ya mionzi ya saratani (chemotherapy) ya mdomo. upande wa juu, ninashukuru sana kwamba bado ninatibika," aliandika kwenye Instagram mnamo 17 Septemba.