Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YA KWANZA KUTUNUKIWA TUZO KWA HUDUMA ZA KIISLAMU AFRIKA MASHARIKI


Mwenyekiti wa Global Islamic Finance Awards (GIFA), Profesa Humayon Dar (kushoto) akikabidhi tuzo ya huduma bora za zinazofuata misingi ya dini ya kiislamu ‘the Best Upcoming Islamic Banking Window 2023’ kwa Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati Benki ya CRDB, Bonaventure Paul (kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki za Kiislamu Benki ya CRDB, Rashid Rashid (katikati) iliyotolewa katika hafla ya 13 ya Global Islamic Finance Awards iliyofanyika katika Hoteli ya King Fahd Palace jijini Dakar, Senegal hivi karibuni.

====== ====== =======


Dar es Salaam. Tarehe 20 Septemba 2023: Ikiwa ni siku chache baada ya kuzindua kadi za Akaunti ya Al Barakah, Benki ya CRDB imekuwa benki ya kwanza katika ukanda wa Afrika ya Mashariki kutunukiwa tuzo ya ubora katika huduma za benki zinazofuata misingi ya sharia mwaka 2023 katika hafla ya 13 ya tuzo za Global Islamic Finance Awards (GIFA) iliyofanyika katika Hoteli ya King Fahd Palace jijini Dakar, Senegal.


Benki ya CRDB imepata tuzo hiyo ikiwa ni miaka miwili tangu Benki ya CRDB izindue dirisha la huduma za kibenki zinazofuata masharti ya Kiislamu “CRDB Al Barakah”. Akikabidhi tuzo hiyo, Mwenyekiti wa GIFA, Profesa Humayon Dar, amesema CRDB inafungua milango kwa taasisi za fedha Afrika Mashariki kuwahudumia Waislamu ambao wangefurahi kuhudumiwa kwa misingi ya imani yao.


“Benki ya CRDB ni taasisi ya kwanza ya fedha kushinda tuzo zetu. Tunaamini mtakuwa mabalozi wazuri wa kulinadi dirisha hili muhimu katika huduma za kibenki katika kuwahudumia Waislamu katika ukanda huo. Tunaamini tutaendelea kushirikiana kufungua fursa zaidi za mitaji na uwekezaji kwa wananchi mnaowahudumia,” amesema Profesa Dar.
Benki ya CRDB ilizindua huduma za Al Barakah mwishoni mwa mwaka 2021 na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi akawa mteja wa kwanza kufungua akaunti na wiki hivi karibuni benki ilimpa heshima ya kuwa mteja wa kwanza kukabidhiwa kadi ya akaunti hiyo hivyo kufungua milango kwa zaidi ya wateja 70,000 ilionao mpaka sasa.


Mpaka sasa, tayari benki imekopesha zaidi ya shilingi bilioni 90 kupitia dirisha hilo huku ikipokea amana zenye thamani ya shilingi 85 bilioni nchini kote.

Akipokea tuzo hiyo, Paul amesema inawatia moyo kuona kwamba ubunifu wanaoufanya unatambulika kimataifa hivyo akaahidi kwamba watauendeleza ili kukidhimahitajina matarajio ya wateja na wawekezaji wanaowahudumia nchini na nje ya nchi ambako Benki ya CRDB inatoa huduma zake.


“Sisi ndio benki ya kwanza kutoa Islamic banking (huduma za kibenki kwa misingi ya Kiislamu) kupitia mtandao mpana zaidi. Huduma zetu zinapatikana kwenye matawi yetu yote 260. Washindani wetu wanahudumia katika maeneo machache lakini sisi tunafika kwenye mikoa yote,” amesema Paul.
Ukiacha Zanzibar na mikoa yenye idadi kubwa ya Waislamu ukiwamo Tanga, Kigoma, Mtwara Lindi na Tabora pekee, ambako Benki ya CRDB imejielekeza, Paul amesema huduma za Al Barakah zinapatikana hata kwenye mikoa yenye idadi ndogo ya waumini wa dini hii.


Kwa upande wake, Rashid amesema imezoeleka kusikia na kuona benki na taasisi nyingine za fedha zikipata tuzo kutokana na huduma za kawaida zinazotolewa kwa wateja ila sasa ni wakati wa tuzo za huduma za benki zinazozingatia sharia.


“Tulete tuzo za huduma zinazofuata misingi ya sharia ili kuudhihirishia ulimwengu kwamba sekta hii ni kubwa na muhimu kwa uchumina maendeleo ya Tanzania. Kwa tuzo tuliyoipata, ninaamini nchi yetu ipo kwenye nafasi nzuri ya kunufaika na fursa za uwekezaji na uwezeshaji wananchi kwa huduma za fedha zinazofuata sharia,” amesema Rashid.


Tuzo hizi za 13 za GIFA zilizoanzishwa mwaka 2011, zilitolewa mbele ya Rais wa Senegal, Macky Sall na kuhudhuriwa na mamia ya washiriki wakiwamo watafiti, wakurugenzi wa kampunina mashirika ya kimataifa kutoka kila pembe ya dunia kutambua mchango wa washindi wake ambao katika kipindi chote, wanafika zaidi ya 700.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com