Na Mariam Kagenda - Kagera
Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Bukoba-BUWASA kwa kushirikiana na Maabara ya maji Mkoa wa Kagera imeendesha zoezi la kupima ubora wa maji kwenye vyanzo vya chemchemi vinavyotumiwa na wakazi wa kata ya Bakoba Manispaa ya Bukoba.
Mamlaka imeamua kuendesha zoezi hili la upimaji wa ubora wa maji ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanatumia maji safi na salama.
Akiongea baada ya kuchukua sampuli hizo za maji Mwakilishi wa Meneja wa Maabara ya Mkoa wa Kagera Bwana Donatus Makamba amesema kuwa wamefanikiwa kupima jumla ya chemichemi 20 na wanaendelea na utafiti ripoti kamili itakapokamilika itawasilishwa kwenye uongozi wa Kata kwa hatua zaidi.
Aidha naye Msimamizi wa kitengo cha Maabara kutoka BUWASA Bi Amina Bajwa amesema kuwa kwa haraka haraka imeonekana chemichemi hizi siyo salama na kwa asilimia kubwa zimezungukwa na ujenzi holela wa nyumba hali ambayo inapelekea maji hayo kutokuwa safi na salama kwa kuwa vimezungukwa na makazi ya watu na hali ya mazingira ya vyanzo hivyo kutoridhisha.
BUWASA inawatahadharisha wadau wa maeneo hayo kuacha kutumia maji ya kwenye chemichemi hizo kwa matumizi ya nyumbani na kutumia maji ya bomba ambayo ni safi na salama , kwani vipimo vya awali vimeonyesha maji haya kutokuwa na ubora hivyo yanaweza kupelekea wananchi wa maeneo hayo kupata magonjwa ya tumbo na UTI