WIZARA YA MALIASILI YAENDELEA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

Wizara ya Maliasili na Utalii imeshiriki kwenye kikao cha kuandaa machapisho yatakayotumika kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na uharibifu unayofanywa na wanyamapori wakali na waharibifu.


Kikao hicho kinafanyika baada ya Wizara kuingia makubaliano na Shirika la Chakula Duniani FAO (Ofisi ya Tanzania) katika kutekeleza programu maalumu ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori hao


Akifungua kikao hicho leo mkoani Morogoro Mkurugenzi wa Mafunzo na Takwimu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Edward Kohi amesema, kama Serikali nia yao ni kuona wanahifadhi wanyamapori na kupunguza migongano baina ya wanyamapori na binadamu.

“ Na hii tu inaweza ikawezekana kama sisi tukishirikiana vizuri maana sisi tunashughulika na wananchi moja kwa moja. Na ukienda ukakuta mtu amekanyagwa na Tembo nafikiri mnaona hali ilivyo. Lakini lazima tuje na mbinu nyingi mbadala ambazo zitatusaidia kuwasimamia Tembo na kusimamia watu.” amesema.


Aidha, Dkt. Kohi amesema, kitu ambacho wanapaswa kukifiria kwa ukubwa wake ni kumuona mnyama Tembo kama rasilimali inayoweza kuondoa umaskini kwenye jamii na si laana ya kuwafanya watu kuwa maskini.

“ Wizara sasa hivi imeongeza juhudi kubwa sana ya kuutangaza utalii, Kwa kutumia kila aina ya mbinu ambazo zinaweza zikawa sahihi za kuleta wasanii wakubwa duniani kuunga mkono juhudi za Mh.Rais Mama Samia Suluhu kwenye filamu ya Tanzania the Royal Tour.”ameongeza.

Kwa upande wake, Mshauri wa Kitaifa wa Kusaidia usimamizi wa migogoro kati ya wanyamapori na binadamu kutoka Shirika la Chakula Dunjani (FAO), Bi. Beatha Fabian amesema programu hiyo imelenga kusaidia na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori hao.

“Najua kwa nchi yetu tuna hifadhi nyingi sana pamoja na maeneo mengine ya namna hiyo. Na migongano ya wanyama na binadamu haiepukiki. Hivyo Programu hii itasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na changamoto hizi za migongano baina ya binadamu na wanyamapori ” amesema Beatha

Kikao hicho kinachofanyika mkoani Morogoro kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo TAWA, TAWIRI na TANAPA, wengine ni TNRF, Halmashauri ya Same, Mkinga, Lushoto, Korogwe pamoja na wadau kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم