*Tuzo imetolewa na Wachimbaji kutambua Mchango wake
*Madini Scheme Mbioni kuanza
*Sekta ya Madini imekua Sekta Kiongozi - Waziri Mavunde
*Mavunde atoa onyo kwa watoroshaji madini nchini
EPZ Bombambili - Geita
Imeelezwa kuwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko ameacha alama kubwa katika Sekta ya Madini katika kipindi chote alichokuwa Waziri wa Madini na kupelekea mabadiliko makubwa katika sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 23, 2023 na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Madini wakati Dkt. Biteko akifungua rasmi Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya EPZ Bombambili Mkoani Geita.
Akizungumza mara baada ya salaam hizo Dkt. Biteko amesema kuwa masuala yote yaliyozungumzwa na mafanikio hayo katika Sekta ya Madini yametokana usimamizi madhubuti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta hiyo.
Kuhusu Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemtaka afanye kazi kwa bidii na kuwataka wadau wa Sekta ya Madini nchini kumuunga mkono katika utekelezaji wa majukumu yake kila siku.
"Vision 2030, Madini Maisha na Utajiri itachangia kuleta mabadiliko na kupunguza umaskini kwa wananchi wengi nchini, Sekta hii ni moyo wa uchumi wa nchi tuitumie kikamilifu ili kuleta mabadiliko," amesema Dkt. Biteko.
Aidha, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kununua kilo 400 za dhahabu zilizosafiswa katika viwanda vya ndani vya kuchenjua dhahabu nchini. Ameitaka Benki Kuu kuwaunga mkono wachimbaji wa madini nchini ili kuleta tija na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini.
Kwa upande, wake Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa Dkt. Biteko ameifanya Sekta ya Madini imekua Sekta Kiongozi kwenye uchumi wa Nchi. Aidha ameipongeza mkoa wa Geita kwa kuandaa maonesho hayo kuwa yenye tija kwa wananchi wa mkoa wa Geita.
" Nimekuja na Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri ili hadi kufikia mwaka huo tuwe tumefanya tafiti katika eneo lote la nchi ya Tanzania ili wananchi wa waweze kunufaika na rasilimali madini," amesema Waziri Mavunde.
Pia, amesema ifikapo mwezi Oktoba Serikali itakabidhi mashine tano za uchorongaji wa Madini ili ziwe msaada kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amesema maonesho hayo yamefungua fursa za uwekezaji kwa wananchi wanaozunguka maeneo mbalimbali mkoani Geita kwa kubadilisha maisha ya jamii hiyo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Geita Constantine Kanyasu amesema kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Biteko ameacha alama kubwa katika Sekta ya Madini nchini. Aidha , ameongeza kuwa mchango wake utakumbukwa katika nyanja zote hususan katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawekea mazingira rafiki ya uchimbaji na uwekezaji.
Wengine walioshiriki katika ufunguzi huo ni Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Wabunge, Viongozi wa Vyama vya siasa, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Wakuu wa Taasisi za Umma na wadau mbalimbali wa sekta ya madini.