Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAENDELEA KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WA WMA KUSIMAMIA RASILIMALI ZA WANYAMAPORI

 

Na Mwandishi Wetu, IRINGA


Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini kwa kutoa mafunzo kwa Viongozi wa Jumuiya za Uhifadhi wa Wanyamapori (WMAs) za WAGA ( katika Wilaya ya Mufindi) na CHAMWINO (katika Wilaya ya Chamwino)  lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya umuhimu wa  kusimamia rasilimali za wanyamapori hasa katika maeneo ambayo wananchi wametenga maeneo yao kwa ajili ya uhifadhi.


Akizungumza leo mkoani humo, kwenye mafunzo ya viongozi wa WMA za WAGA na Chamwino  kuhusu usimamizi na uendelezaji wa maeneo ya  Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori,  Mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Rose Mdendemi amesema wanatarajia baada ya mafunzo hayo viongozi hao watakuwa na nafasi nzuri za kuendeleza uhifadhi na kusimamia rasilimali katika maeneo  ya Jumuiya hizo.


Bi. Mdendemi amesema mafunzo hayo yamewezeshwa kupitia Mradi wa Kudhibiti Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara (IWT – PROJECT) unaotekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii ambao unalenga Wananchi wanashiriki kikamilifu  katika shughuli za uhifadhi nchini, kudhibiti ujangili,  kupambana na wanyamapori wakali na Waharibifu na kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia shughuli za utalii.


“ Kwa kifupi tunaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika kuendeleza utalii kwa kuwezesha wananchi kuwapatia ujuzi wa namna ya kusimamia maeneo yao ya hifadhi na  kupunguza migongano  baina ya binadamu na wanyamapori wakali na wabaribifu ” amesema.




“Tunawashukuru wenzetu wa UNDP wanatusaidia katika kutekeleza majukumu haya. Tunaamini kupitia mafunzo haya yatawezesha wananchi kusimamia rasilimali hizi vizuri na hatimaye kufikia malengo ya kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa Ujumla.” aliongeza Bi. Mdendemi


 Kwa upande wake, Rachel John Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka wilaya ya Mufindi Pamoja na Afisa Wanyamapori Mkuu wa Wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma, Yusuph Nyonyi wameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo ni muhimu katika jamii zilizotoa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za uhifadhi 



Naye Mwakilishi Kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa  Mataifa (UNDP), Damas Masologo amesema nimatarajio ya Shirika hilo kuwa Mradi utapokuwa umekamilika, Jumuiya mbalimbali za Wanyamapori nchini zitakuwa zimesimama vizuri  hasa katika kutekeleza majukumu yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com