MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Tehama nchini(ICTC) Dk.Nkundwe Mwasaga,akizungumza kuelekea kongamano kubwa la saba litakalofanyika Oktoba 16 hadi 20, 2023 jijini Dar es salaam.
Na Mwandishi Wetu
TUME ya Tehama nchini(ICTC) imewaalika wadau wa Tehama kushiriki katika kongamano kubwa la saba litakalofanyika Oktoba 16 hadi 20, 2023 jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dk.Nkundwe Mwasaga, amesema kongamano hilo litakuwa la siku tano ikiwamo siku mbili za mijadala mahsusi inayolenga kuchochea uchumi wa kidigitali wa sasa.
“Uchumi wa kidigitali unapaswa kuwa jumuishi, yaani watu wa makundi mbalimbali wanufaike na mapinduzi haya ya Tehama, siku ya kwanza ya kongamano itakuwa ni siku ya wanawake kwenye Tehama ambayo itajadili maendeleo ya Tehama yanavyogusa wanawake tunasherehekea maendeleo makubwa waliyoyapata wanawake na kujadili changamoto zinazowakumba kwenye tasnia hii ili twende kwa pamoja,”amesema.
Amesema siku ya pili ya mjadala itakuwa ya vijana kwa kuangalia mafanikio na vikwazo vinavyowakabili.
“Kutakuwa na mada mbalimbali zitakazojadiliwa, mada moja wapo duniani kote wanaangalia kwa makini matumizi ya teknolojia chipukizi, tutaangalia jinsi gani teknolojia za namna hii zinavyoweza kuleta maendeleo kwa wanawake na vijana,”amesema.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa za sensa 2022, vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 34 ni takribani watu milioni 21 na kusisitiza kuwa vijana ndio wanaotegemewa wawe watumiaji wakubwa kutokana na uchumi wa kidigitali.
“Ni muhimu kuja kuwasikiliza tujadiliane kwa pamoja tujue ni changamoto gani wanazokutana nazo ili kuhakikisha nchi yetu inakwenda vizuri,”amesema.
Dk. Mwasaga amesema miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo ni watalaamu wa Tehama kutoka Misri, Estonia, Kenya na maeneo mengine.
“Moja ya teknolojia ibukizi ambazo tutajadili ni akili bandia, hii ni fursa iliyopo duniani na katika teknolojia mpya zinazojitokeza inatakiwa watu waandaliwe ili wawe na uwezo wafanye ubunifu na zitengeneze kazi na kuchangia pato la taifa,”amesema.
Amewaalika wadau mbalimbali kutumia fursa ya kushiriki kwenye kongamano hilo ili kuonesha teknolojia na bunifu wanazofanya.
“Nitoe wito kwa wadhamini mbalimbali wa kongamano bado nafasi zipo wadhamini waje wadhamini kongamano liendelee kuwa na sura ya kimataifa,”amesema.
Ili kushiriki kongamano hili, tafadhali wasiliana kupitia www.taic@ictc.go.tz au info@ictc.go.tz , au simu namba 0738171742 au ingia kwenye Tovuti: www.ictc.go.tz
Social Plugin