Safari Manjala enzi za uhai wake
Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Mkulima na mfanyabiashara maarufu wa Tumbaku Safari Manjala (54) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Ulowa na Mmiliki wa Manjala Station na Manjala Logde anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi akitumia bunduki yake aina ya Bastola akiwa kwenye shamba la miti yake katika kijiji cha Ilomelo kata ya Ulowa halmashauri ya Ushetu wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Malunde 1 blog kuwa, tukio hilo limetokea leo Ijumaa Septemba 8, 2023 majira ya saa mbili asubuhi ambapo Safari Manjala mkazi wa Kitongoji Namba Tisa A kijiji cha Ilomelo kata ya Ulowa anadaiwa kujipiga risasi mbili kidevuni na risasi kutokea kichwani.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema Safari Manjala ambaye ni mmiliki wa Manjala Lodge, Manjala Petrol Station na Mwenyekiti wa Wazazi CCM Kata ya Ulowa ameamka akiwa mzima na baada ya hapo alielekea kwenye msitu wake kisha akajipiga risasi na kwamba chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Diwani wa Kata ya Ulowa Mhe. Gabriella Alphonce Kimaro amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akiwaomba wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi/maamuzi magumu pindi wanapokuwa na msongo wa mawazo na badala yake watafute ushauri kwa watu wa karibu au viongozi.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kahama, bw. Hassan Ramadhani amesema CCM Kahama imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Safari Manjala ambaye amekuwa mwanachama wa muda mrefu wa CCM lakini pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi kata ya Ulowa huku akiongeza kuwa mpaka sasa chanzo cha Safari kuchukua maamuzi ya kujitoa uhai bado hakijajulikana.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa amesema Chama kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo huku akieleza kuwa Chama kimepoteza mwanachama/kiongozi ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika chama na jamii huku akibainisha kuwa taarifa zaidi kuhusu msiba huo zitaendelea kutolewa.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Kennedy Mgani amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
"Jeshi la polisi limepokea taarifa za tukio hilo, askari polisi wetu wamefika katika eneo la tukio",amesema .