WANAFUNZI NYAMKUMBU WANOLEWA NA GGML KUHUSU TAALUMA YA MADINI

Israel Ryoba, Mtaalamu wa Usafi Kazini kutoka Idara ya Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo kutoka GGML akiwapatia maelezo wanafunzi wa shule ya sekondari Nyankumbu kuhusu sera za afya na usalama mahala pa kazi.
Regina Mabula, Afisa Maendeleo ya uchumi wa jamii, kutoka GGML, akiwapatia maelezo wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu kuhusu mchoro wa 3D wa Uwanja wa Magogo ambao ni moja ya miradi inayofadhiliwa na GGML katika ujenzi wake.
El-Cid Walter, Ofisa kutoka idara ya Usalama mahala pa kazi, HSE&T akiwaelezea wanafunzi wa shule ya sekondari Nyankumnbu mbinu za usalama zilizoiwezesha kampuni hiyo kushinda tuzo za afya na usalama mahala pa kazi.
Israel Ryoba, Mtaalamu wa masuala ya usafi kazini kutoka Idara ya Afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo ya GGML, akiwapa maelezo wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu kuhusu sera ya kampuni inayoiongoza katika sekta ya afya kazini.


Na Mwandishi Wetu

ZAIDI ya Wanafunzi 50 kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu iliyopo mkoani Geita wamepatiwa mbinu za kuzingatia katika masomo yao ili kukua kitaaluma na kuja kuwa watalaamu wa masuala ya madini baadae.


Wanafunzi hao wamepatiwa elimu na uzoefu huo jana kutoka kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) walipotembela banda la kampuni hiyo katika maoneosho ya sita ya teknolojia ya madini yanayoendelea kwenye viwanja vya Bombambili-EPZ Mjini Geita


Wanafunzi hao wanaosoma masomo ya mchepuo wa sayansi, walipata fursa ya kutangamana na wafanyakazi wa GGML na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu shughuli za uchimbaji madini kama vile utafiti, uchimbaji, uendelezaji na usimamizi wa mazingira.


Pia walijifunza namna kampuni hiyo inavyoshirikiana na Serikali katika kutekeleza sera ya maendeleo ya jamii na kuzingatia sheria ya afya na usalama kazini.


Pamoja na mambo mengine walipewa taarifa kuhusu ufadhili wa masomo unaopatikana kwa vijana wa kike wanaotaka kusomea masuala yanayohusu sekta ya madini na namna nafasi za kazi zinavyopatikana ndani ya kampuni hiyo.

Akizungumzia ziara hiyo Meneja Mwandamizi anayeshughulikia mahusiano ya jamii kutoka GGML, Gilbert Mworia, alisema ni moja ya mbinu muhimu kwa wanafunzi hao kujifunza na kupata uzoefu kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni.


Aliongeza kuwa ni sehemu ya jitihada GGML kuendelea kukuza elimu na maendeleo ya kitaaluma kwa vijana wa mkoa wa Geita hususani wasichana.

“GGML ni mdau muhimu pia katika masuala ya elimu hasa ikizingatiwa ndio iliyoanzisha na kusaidia maendeleo ya shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu ambayo sasa ni shule kubwa ya sekondari ya wasichana mkoani Geita iliyofunguliwa rasmi mwaka 2014."

“Haya ni matokeo ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ambapo GGML ilifadhili ujenzi wa shule hiyo kisha Halmashauri ya Mji wa Geita ikatoa ardhi,” alisema.

Alisema katika uanzishwaji wa shule hiyo, Serikali kuu ilichukua jukumu la usimamizi wa kila siku, kuweka mazingira salama kwa wasichana hao wadogo kupata maarifa na ujuzi wanaohitaji ili kuja kuwa watalaamu mbalimbali hapo baadae.


Aliongeza kuwa katika kampuni hiyo ambayo pia ni mdhamini mkuu wa maonesho hayo ambayo hufanyika kila mwaka mkoani Geita, imekuwa ikishiriki maonesho hayo kwa lengo la kuonesha ubunifu na mbinu bora za kisasa zinazotumiwa na kampuni hiyo kwenye sekta ya uchimbaji madini.


"Tunafuraha kuwakaribisha wanafunzi hawa mahiri na wenye vipaji kwenye banda letu na kushirikiana nao uzoefu wetu kwenye sekta ya uchimbaji madini,” alisema Mworia.


Aidha, Afisa Maendeleo ya Uchumi wa Jamii kutoka wa GGML, Regina Mabula alisema; “Tunatumaini kuwa ziara hii itawatia moyo katika kutimiza malengo yao ya kitaaluma na kufikiria kujiunga na taaluma ya uchimbaji madini”.


Pia aliwashukuru walimu na wafanyakazi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu kwa ushirikiano na kuwaruhusu wanafunzi hao kuja kwenye maonesho hayo.


“Tunathamini ushirikiano wetu na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu na tunatarajia kuendelea kusaidia programu zao za elimu kwa sababu tunaamini kuwa kuwekeza katika elimu ni kuwekeza katika mustakabali wa maisha ya jamii yetu na nchi kwa ujumla,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post