KENYA NA CHINA ZAVUTIWA NA FURSA ZA UWEKEZAJI KWENYE MIFUGO

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Ranchi ya Mbogo Bw. Naweed Mullah (kulia) akimuongoza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Dkt. Daniel Mushi (kushoto) na timu ya washiriki wa  Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula  (AGRF) waliofika shambani kwake Chalinze, Septemba 03,2023 kwa ajili ya kuona namna anavyofanya shughuli zake.
Meneja Uendelezaji biashara kutoka kiwanda cha kusindika nyama cha "TANCHOICE" Bw. Luwungo Hassan (aliyesimama mbele) akielezea kwa ufupi historia ya kiwanda hicho kwa washiriki wa Mkutano wa Jukwa la mifumo ya Chakula (AGRF) waliofika kiwandani hapo Septemba 03, 2023.
Sehemu ya aina ya Ng'ombe waliopo kwenye ranchi ya Mbogo iliyopo Chalinze mkoani Pwani.


 ◾Ni mara baada ya kuwatembelea wadau wa Sekta hiyo..


Nchi za China na Kenya zimeonekana kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo kwenye sekta ya Mifugo mara baada ya kuwatembelea wawekezaji wa ndani ambao ni Ranchi ya Mbogo na Kiwanda cha kuchakata nyama cha “Tanchoice” vilivyopo mkoani Pwani Septemba 03, 2023.

Ziara hiyo ambayo ni miongoni mwa shughuli za utangulizi zinazofanyika kabla ya kufanyika kwa mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya chakula barani  Afrika (AGRF) iliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo Dkt. Daniel Mushi ambapo alibainisha kuwa Wizara yake imejiandaa kikamilifu kutumia fursa zitakazojitokeza katika pindi chote cha mkutano huo kuiimarisha sekta ya Mifugo nchini.

“Sisi kwa sasa kama nchi tunasema  “flagship” ya wizara yetu ni nyama na samaki ambazo tunazipeleka nje ya nchi na kwa mwaka jana tulifanikiwa kusafirisha tani elfu 14 na malengo yetu ni kuvuka tani elfu 16 kwa mwaka huu wa fedha na hilo tunaweza kufanikiwa kwa kuleta wadau wengi zaidi kama mbogo ranchi” Amesema Dkt. Mushi.

Aidha Dkt. Mushi ameongeza kuwa lengo la mkutano huo ni kupata wawekezaji na masoko mapya ili nyama inayozalishwa nchini iweze kuuzwa kwa wingi nje ya nchi hatua ambayo anaamini itachangia ongezeko la fedha za kigeni kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa ranchi ya Mbogo Bw. Naweed Mullah amesema kuwa anatarajia kutumia mkutano huo wa kimataifa wa jukwaa la Mifumo ya chakula kuhakikisha anatoa elimu ya kutosha kwa washiriki wa ndani na nje ya nchi kuhusu njia bora za uongezaji thamani wa ng;ombe wa asili waliopo hapa nchini na barani Afrika kwa ujumla.

“Tunajua ulimwengu mzima unakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula hasa nyama na hali ya upatikanaji wa zao hilo imeendelea kushuka kutokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo tunaamini jukwaa hili limelenga kujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto hiyo” Ameongeza Bw. Mulllah.

Naye mmoja wa washiriki wa ziara hiyo Bi. Wangari Kurya kutoka nchini Kenya mbali na kukoshwa na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya Mifugo nchini amevutiwa zaidi na namna Serikali inavyohamasisha aina zote za kilimo ikiwa ni tofauti na kwao ambako kilimo mazao ndio kimekuwa kikisisitizwa zaidi.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya “FAMSUN” kutoka nchini China Bw. Joy Lee amevutiwa na namna Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na ardhi kubwa na nzuri kwa ajili ya kufanya shughuli za ufugaji tofauti na hali ilivyo nchini kwao ambako wanalazimika kutumia kiwango kikubwa cha teknolojia ili kutekeleza shughuli hizo kwenye maeneo madogo waliyonayo.

“Ninatoa wito kwa wawekezaji wote kuja Tanzania kuna fursa nyingi sana za uwekezaji kwa upande wa sekta ya Mifugo” Amehitimisha Bw. Lee.

Mkutano wa Jukwaa la kujadili Mifumo ya chakula barani Afrika unatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia Septemba 05-08, 2023 ambapo takribani 6000 wa ndani na nje ya nchi  wanatarajia kushiriki kwenye mkutano huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post