Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KWAYA YA MWENYEHERI MARIA THERESA LEOCHOWSKA KIWANJA CHA NDEGE DODOMA YAWAITA WATANZANIA TAMASHA LA UIMBAJI





Mwenyekiti wa kwaya ya Mwenyeheri Maria Theresa Leochowska, Dk.Paul Loisulie,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya zoezi la utoaji damu katika kuelekea kwenye uzinduzi tamasha la uimbaji wa nyimbo za Injili,Oktoba 22 Mwaka huu jijini Dodoma.


Na Alex Sonna-DODOMA


Kuelekea uzinduzi wa tamasha la uimbaji wa nyimbo za injili,Oktoba 22 mwaka huu,waumini wa Parokia ya Kiwanja cha Ndege wamechangia damu huku wakiwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo.


Akizungumza na Waandishi Habari wakati wa zoezi la utoaji wa damu, Mwenyekiti wa kwaya ya Mwenyeheri Maria Theresa Leochowska, Dk.Paul Loisulie, amesema katika kuadhimisha miaka 27 tangu kuzaliwa kwa kwaya hiyo watafanya tamasha kubwa ambalo watashiriki waimbaji mbalimbali.


Amesema kuelekea tamasha hilo kuna matukio ambayo wameyandaa kama shukrani ya kuwaweka pamoja hai na kumshukuru Mungu kwa miaka 27.


Amesema tukio mojawapo ni kujitolea damu kama sadaka hivyo wameshirikiana na Hospitali ya Benjamini Mkapa hasa waumini wa Parokia ya Kiwanja cha ndege kwa kutoa damu ambayo itaokoa maisha ya watanzania.


"Kitendo hichi ni kama shukrani kwa Mungu kwa kutuweka hai na tunapofikia kilele Oktoba 22 tuna amani kuna mambo tumefanya kwa sababu hawa watu wanaoimba ni binadamu hivyo ni lazima ili kushiriki katika matukio mbalimbali ya kijamii,"amesema


Amesema malengo waliyoweka ni kuhamasisha watu wengi kujitokeza kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watanzania.


Amesema pia wameweka mikakati katika suala la mazingira na maadili kwa kutunga nyimbo ambazo zitazinduliwa siku ya kilele.


"Tunalenga kuna vitu vinaisumbua jamii ili sisi tuweze kuimba vizuri ni lazima watu wawe na afya waishi katika mazingira mazuri na wawe na maadili na tumeishaenda katika Gereza la Isanga kwa ajili ya kuwatembelea wafungwa,"amesema


Pia Mwenyekiti Loisulie ameitaka Jamii kuungana katika matendo ya huruma ikiwa ni pamoja na kutoa damu kwa watu wengine.


"Niwaombe tarehe 22 wahudhurue katika tamasha,wakishiriki watakuwa wameshiriki katika masuala ya mazingira na maadili na kutafakari maisha yetu bila kujali dini,wala kabila,tunawakaribisha sana.


"Tunaona namna ambayo mmonyoko wa maadili unaisumbua jamii na mengine mengi tunataka tuwe sehemu ya kupaza sauti kupitia uimbaji,"amesema


Amesema mgeni rasmi siku ya kilele anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi Mstaafu Generali Venance Mabeyo


Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha Damu Salama, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Kucy Kibaja, amesema wakati zoezi hilo likiendelea wamepata chupa za damu 66.

Ametoa rai kwa watanzania wengine kuiga mfano huo uliofanywa na waumini hao.


"Nenda kachangie chupa moja ambayo inaokoa maisha ya kuanzia watu wawili mpaka watatu.Nawaomba watanzania tembeleeeni vituo vya damu salama ili kujitolea damu ili iokoe maisha ya watanzania,"amesema


Naye, Mchangia damu,Rachel Mrema ameomba watanzania kujitokeza kujitolea damu kwani mahitaji ni makubwa kwenye jamii.


"Kuchangia damu ni jambo zuri na tunapaswa kuwa ni utaratibu wa kawaida kwetu,"amesema Rachel




WANAKWAYA wa Mwenyeheri Maria Theresa Leochowska,Parokia ya Kiwanja cha Ndege wakichangia damu kuelekea kuadhimisha miaka 27 tangu kuzaliwa kwa kwaya hiyo watafanya tamasha kubwa ambalo watashiriki waimbaji mbalimbali Oktoba 22 jijini Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com