Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAVUNDE AITAKA TEITI KUWA KITOVU CHA TAARIFA ZA MADINI


Na Mwandishi wetu -Dodoma


Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameitaka Taasisi ya Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini (TEITI) kuwa kitovu cha taarifa za rasilimali madini ili kuisadia serikali na Wizara katika ukusanyaji wa mapato kutoka katika rasilimali za hiyo ili kuongeza tija katika mnyororo mzima wa sekta ya madini nchini.

Waziri Mavunde ametoa maelekezo hayo leo septemba 12, 2023 wakati akizungumza katika kikao na TEITI pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), kikao kilichofanyika jijini Dodoma.


Mhe . Mavunde amesema TEITI ina jukumu kubwa la kukusanya taarifa na takwimu zinahusu rasilimali madini hivyo ni matarajio kuwa taarifa au takwimu hizo zitasaidia Wizara katika mipango yake ya kuongeza mapato.


“Sekta hii ni kubwa sana, ili kufikia lengo la kuongeza mapato ya serikali tunapaswa kuwa na taarifa sahihi zilizofanyiwa utafiti pamoja na takwimu sahihi za mapato ambazo zitaiongoza wizara kujua ni eneo gani linapaswa kuongezewa nguvu zaidi hii ni kutokana na TEITI yenyewe kuwa ni kitovu cha taarifa zote zinazohusu rasilimali madini" amesema Mavunde.


Akizungumzia kuhusu TGC, Waziri Mavunde amekitaka kituo hicho kusaidia Wizara kufikia lengo la kuongeza thamani madini ili kutimiza lengo la kuanzishwa pamoja kuyafanyia kazi yale mliyojifunza katika ziara ya China na Thailand


“Nimesikia kuwa mlitembelea nchi ya China na Thailand, ni matumaini yangu kuwa mtayafanyia kazi yale mliyojifunza huko, ujuzi huo mlioupata huko tuone ukipatikana hapa ndani ya nchi na tuwajengee uwezo watu wetu ili wafanye vizuri zaidi katika eneo hilo la kuongeza thamani madini yetu” amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema lengo la kuanzishwa kwa TEITI ni kuhakikisha wizara inakuwa na Takwimu sahihi zinazohusu rasilimali Madini ili zisadie katika kufikia malengo yake yakiwemo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TEITI, Mariam Mgaya amesema kuwa TEITI imepanga kuweka wazi mikataba ya serikali na makampuni yaliyowekeza katika rasilimali zao ili kuweka uwazi wa mikataba hiyo.


Ameongeza kuwa TEITI inatarajia kuweka wazi kiasi cha hisa za serikali kwa kampuni zinazoingia nayo ubia hapa nchini ili wananchi wafahamu mawanda ya umiliki wa hisa ya serikali katika kampuni hizo na manufaa yanayopatikana.


Pia, ameeleza kuwa TEITI imepanga kufanya Tafiti kwenye shughuli za sekta ya madini ili kuweka wazi kuhusu uharibifu wa mazingira sambamba na mchango wa wachimbaji wadogo katika sekta ya madini ambao kwa siku za karibuni umeongezeka sana.

Akizungumza Kwa niaba ya Mratibu wa TGC, Kaimu Mratibu Msaidizi, Kurugenzi ya Mipango, Tafiti na Uendelezaji Ujuzi wa kituo hicho, Jumanne Shimba amesema kuwa kituo hicho kimepanga kuwa na maabara yenye viwango vya kimataifa ili kutoa huduma za uongezaji thamani madini kwa viwango vya kisasa


Pia amesema kuwa kituo hicho kimepanga kuanzisha vituo ambavyo vitatangaza fursa ya Madini nchini ambapo mpaka sasa tayari wameishaanza katika kiwanja kimoja cha ndege ambacho ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na mipango mingine ikiendelea katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere (JNIA) na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com