Na Halima Khoya, SHINYANGA
MWANAFUNZI mwenye umri wa miaka 18 Mkazi wa Lyabukande Tarafa ya Itwangi Mkoa Shinyanga (Jina lake limehifadhiwa) anatuhumiwa kutoa mimba changa kwa kunywa dawa za ukame.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi amesema alipata taarifa hizo tarehe 12.09.2023 majira ya saa nne usiku ambapo aliyemuuzia dawa amekamatwa pamoja na mwanaume ambaye amempatia ujauzito.
Magomi amesema Mwanafunzi huyo amepelekwa hospitali ya Rufaa Mwawaza kwa ajili ya matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na yupo chini ya ulinzi wa Jeshi hilo.
“Tunathibitisha kupokea taarifa ya binti aliyetoa mimba Tarehe 12.09.2023 majira ya saa nne usiku (Jina lake limehifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Lyabukande Tarafa ya Itwangi, pia tunamshikilia muuza duka la dawa na mtia mimba” ,amesema Magomi.
Hata hivyo Magomi amewaasa wanafunzi kufahamu kuwa wazazi wanatumia nguvu nyingi kuwasomesha wakiwa na matarajio ya kuwasaidia hapo baadae na kwamba Jeshi la Polisi Shinyanga linaendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wakishirikiana na taasisi mbali mbali (NGO’S).
“Niwaombe viongozi wa dini tuendelee kutoa elimu za ukatili wa kijinsia kwa watoto wetu kupitia mahubiri,watoto wakike muache kiburi ambacho kinasababisha kuangukia pabaya” ameongeza.
Social Plugin