WAHITIMU (Alumni) ni Rasilimali muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya Vyuo Vikuu mbalimbali duniani ikiwemo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Hayo yamesemwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, pembeni ya kikao cha Baraza la Seneti kilichoketi Septemba 18, 2023 Makao Makuu ya Chuo, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
"Wahitimu ni wadau wakubwa katika kuleta chachu ya maendeleo katika Chuo chetu kwani kupitia wao tunaweza kupata mrejesho wa kile wanachofanya na kuboresha mitaala yetu kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ajira. Pia, Alumni ni mabalozi na wajumbe wa kukisemea vizuri Chuo na kukifanya kifahamike kwa jamii na kisha kutoa mchango wake wa kukuza na kuendeleza Rasilimali watu kwa maendeleo ya Taifa letu." Amesema Prof. Bisanda.
Kutokana na umuhimu wa Alumni, Prof. Bisanda, amesema Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimepanga kufanya Mkutano mkubwa wa Alumni wote utakaofanyika Septemba 21, 2023 jijini Dodoma kwenye Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania cha jijini hapo, kuanzia Saa Mbili Kamili Asubuhi.
Kupitia Mkutano huu Alumni wote watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kutoa mrejesho wa namna gani masomo waliyosoma yamewasaidia katika soko la ajira, kutoa huduma bora kwa wananchi na changamoto walizokumbana nazo ili tuendelee kuimarisha mtaala hasa katika kipindi hiki ambapo tunaendelea na kazi ya Mapitio ya Mitaala ya programu zetu zote.
Prof. Bisanda ametumia fursa hii pia kuwaalika Alumni wote kushiriki mkutano huo adhimu ambao utakuwa na mambo mengi mazuri yakiwemo ya uchaguzi wa viongozi na kupanga mikakati ya kuendeleza Chama cha Alumni cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.