Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAITAKA TRC KUTUMIA MAKASHA YA UBARIDI KUHAKIKISHA KUNAKUWA NA USAFIRISHWAJI ENDELEVU WA MAZAO YA MATUNDA NA MBOGAMBOGA



Na Mwandishi wetu - Dar es Salaama

Serikali imelitaka Shirika la Reli Tanzania(TRC) kutumia makasha ya ubaridi kuhakikisha kunakuwa na usafirishaji endelevu wa mazao ya mbogamboga na matunda Nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa wakati wa hafla ya makabidhiano ya Makasha 5 ya ubaridi kati ya Shirika la reli Tanzania (TRC) na Shirika la Mpango wa chakula Duniani(WFP) yaliyofanyika kwenye eneo la upakiaji na upakuaji wa bidhaa la TRC lililopo Ilala Jijini Dar es salaam.

Prof Mbarawa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imejipanga kuifungua nchi kimataifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii,biashara, kilimo na miundombinu ya usafirishaji hivyo upokeaji wa makasha haya utahakikisha wakulima wa mazao ya matunda na mbogamboga kutoka mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Dodoma wanaondokana na adha za usafirishaji wa mazao yao ndani na nje ya nchi kwa ubora ule ule toka kwenye eneo la uzalishaji mpaka kumfikia mlaji na kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa.
“Makasha haya ya ubaridi ni ukombozi mkubwa kwa wakulima wa mbogamboga na matunda kwani yatapunguza hasara zilizokuwa zikipatikana hapo awali kwa wakulima kukosa namna bora ya uhifadhina usafirishaji wa mazao haya, hivyo naitaka TRC kuhakikisha kunakuwa na usafirishaji endelevu wa mazao haya kuanzia sasa,mabehewa haya yatunzwe na kuongeza mabehewa ili kufikia mikoa zaidi kwa kadri ya ufanisi”, amesisitiza Prof Mbarawa
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Chakula Duniani kwa upande wa Tanzania Bi Sarah Gordon amesema ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya shirika hilo na Serikali ya Tanzania kupitia TRC ndiyo uliopelekea makabidhiano haya ya makasha matano ya ubaridi yenye thamani ya dola za Kimarekeni 337,000 sawa na shilingi Bil 840 za kitanzania ikiwa ni mkakati wa kukuza na kuendeleza kilimo cha mbogamboga na matunda Tanzania,kupunguza hasara kwa wakulima na kusaidia ukuaji jumuishi wa uchumi wa nchi.


“Asilimia 40 ya mazao haya hupotea katika mnyororo wa kutokea kwa mzalishaji mpaka kufika kwa mlaji kwa sababau ya kukosekana njia sahihi za uhifadhi na usafirishaji,makasha haya ya ubaridi yatasaidia bidhaa kupozwa kuanzia mahali ilipozalishwa mpaka inafika sokoni na kwa gharama nafuu hivyo kuongeza thamani na mapato kwa wakulima na shirika litatia mkazo kwa vijana washiriki zaidi kwenye biashara hii kwani inafaida ya haraka” amesisitiza Bi Sarah


Katibu Mkuu Wizari ya Kilimo, Gerard Mweli amesema uzalishwaji wa mazao ya mbogamboga na matunda nchini umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka licha ya changamoto zilizokuwepo kwani kwa mwaka 2022-2023 uzalishaji ulikuwa ni metric tani Mil 8 likiwa ni ongezeko kutoka metric tani mil 6.5 kwa mwaka 2017-2018 na kwa mipango iliyopo kwa sasa tunatarajia kufikisha metric tani Mil 25 ifikapo mwaka 2030 na kutoa wito kwa wadau kujitokeza kuwekeza zaidi kwenye eneo la uhifadhi na usafirishaji kwa njia ya ubaridi.

Mhe Mweli ameongeza upokeaji wa Makasha haya ya ubaridi ni eneo la kwanza la jitihada za Serikali kuinua kilimo eneo la pili ni ujengwaji wa mabwawa ya umwagiliaji maeneo ya Mpwapwa inapopita reli ya kati na la tatu ni hekali 5 ambazo zimeshapatikana bandarini kwa ajili ya kuanzisha green belt pale bandarini kwa ajili ya uhifadhi wa mazao haya kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.


Akitoa salamu za Shirika,kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania amemshukuru Serikali ya awamu ya sita na Wizara ya Uchukuzi kwa mahusiano inayoyaendeleza na mashirika ya kimataifa ambayo yamefanikisha makabidhiano haya ya makasha ya ubaridi ambayo yataongeza tija kwenye bidhaa zetu ndani na kimataifa na kumkomboa mkulima na kuongeza kuwa kwa kuanzia shirika litaanza na mikoa ya Dar es salaam,Dodoma na Morogoro na baadae kuendelea Arusha, Mwanza, kigoma na Tabora ili kuwafikia hata wafugaji na wavuvi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com