Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TMX YAJIPANGA KUBORESHA MFUMO WA KIELEKTRONIKI ILI KUONGEZA BIDHAA ZAIDI KWA AJILI YA MAUZO



Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Bidhaa Nchini (TMX) , Bw.Godfrey Malekano akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari nchini leo Septemba 7,2023 Jijini Dar es Salaam.

****************

Na Beatrice Sanga-MAELEZO

Soko la Bidhaa Nchini (TMX) limejipanga kuimarisha mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha utendaji kazi wa soko hilo na bidhaa mbalimbali zinazouzwa kupitia soko hilo zikiwemo za Kilimo, Madini, Mifugo, nishati.

Hayo yamebainishwa Septemba 7, 2023 na Godfrey Malekano Afisa Mtendaji Mkuu wa soko hilo wakati wa Mkutano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, na wahariri wa Vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa TMX imejipanga kuwa Soko linaloongoza, anuwai zaidi na linalokwenda na wakati katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Amesema ili kutimiza adhima hiyo Soko hilo halina budi kuboresha mifumo ya kieletroniki ili kuongeza bidhaa zaidi kwaajili ya masoko, kutoa huduma za kisasa, zenye ufanisi kwa uwazi na uadilifu kupitia jukwaa la kuaminika la mauzo ya bidhaa kwa njia ya teknolojia ya hali ya juu katika kutekeleza na kutimiza malengo ya maendeleo ya Taifa.

“Mfumo wa Kielektroniki unaendelea kuboreshwa kuongeza bidhaa zaidi kwa ajili ya mauzo, Mfumo wa Kielektroniki wa TMX unaweza kuhusisha “Reverse auctions” ambapo wanunuzi wanaweza kutangaza kununua kiasi fulani cha bidhaa ya daraja maalum katika eneo maalum la kuwasilisha, na wauzaji kushindana kwa bei kwenye mfumo wakati wa mauzo (trade sessions),” amesema Malekano

Kwa sasa Soko hilo nchini limewekeza katika teknolojia mbalimbali katika Soko la Bidhaa ikiwemo Mabango ya kidigitali ya kusambaza taarifa za mauzo, Uwekezaji katika Soko la Bidhaa-Trading Floor, Uwekezaji katika Soko la Bidhaa-Data Centre ambapo linashirikiana na Benki Nane (8) ambazo zimekuwa zikifanya Malipo kwa kiasi kikubwa.

“Mabango ya Kidijitali (Electronic Display Units) yanaendelea kuwekwa katika baadhi ya maeneo ya kimkakati kwa ajili ya usambazaji wa taarifa za bei na soko kwa wadau na umma, hivyo Mfumo wa Kielektroniki umetengenezwa katika njia ambayo wadau wanashiriki popote walipo.” Amongeza Malekano.

Mtendaji Mkuu huyo amesema TMX watajitahidi kuendelea kushirikiana na kufanya kazi na masoko mengine makubwa ya bidhaa duniani kwaajili ya kupata uzoefu na ujuzi zaidi katika kuendesha soko hilo, ikiwemo Nasdaq Futures na London International Financial Futures Exchange (LIFFE), soko la Bidhaa la Ethiopia, Soko la Bidhaa la Ghana, MCX na NCDEX India.

Aidha TMX kwa sasa limeendelea na Uhamasishaji na program za mafunzo mbalimbali kwa wadau ikiwa ni pamoja na wakulima, wanunuzi, wenye viwanda, taasisi za fedha, watunga sera na wasimamizi ambapo mpaka zaidi ya wadau 190,000 wamefikiwa kwenye mikoa 25 ya Tanzania kuanzia mwaka 2018.

“Tathmini ya mnyororo wa thamani wa biashara umefanyika (ufuta, choroko, kakao, dengu, korosho, Pamba, mifugo, chai, kahawa), huku bidhaa mbalimbali zinaendelea kufanya vyema sokoni ikiwemo iliki, mbaazi, mkonge, mifugo hai, nyama, ngozi, nyanya, vitunguu na ndizi.” Amefafanua Malekano.

Soko la Bidhaa Tanzania ni mfumo rasmi unaokutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja na kufanya biashara ya mikataba ya bidhaa, inayotoa uhakika wa ubora, ujazo na malipo ambapo Soko hilo huleta wanunuzi wengi wa ndani na nje ya nchi ambao sio lazima wafike kwenye soko la bidhaa au nchini kwa kuwa mauzo katika Soko la Bidhaa hufanyika kwa kutumia Mfumo wa Kidijitali ambao huwawezesha wanunuzi wa bidhaa kufanya manunuzi popote walipo ndani na nje ya nchi.

Soko la bidhaa limekuwa na mchango mkubwa kwa wauzaji, wanunuaji na serikali kwa ujumla ikiwemo kuimarisha bei ya soko, upatikanaji wa taarifa za soko, kuvumbua bei za bidhaa, kupunguza gharama za kuuza na kununua, wakulima wako huru kuamua bei walioridhia kuuza bidhaa zao, imekuwa ni njia rahisi ya kukusanya mapato kwa Halmashauri, lakini pia urahisi wa Usimamizi wa utoaji wa vibali husika kwa usafirishaji wa bidhaa zilizouzwa, imesaidia upatikanaji wa Fedha za Kigeni (FOREX).

Kwa sasa soko hilo limejipanga kutoa elimu na kuwafikia wadau wengi zaidi ili wafahamu mchango wake katika uchumi wa nchi, kujiendesha kwa ufanisi, kidijitali na kutoa huduma zake kwa uadilifu ili kulinda maslahi ya washiriki wake wote, kufanya utafiti kwa kushirikiana na wadau husika ili kuongeza bidhaa zaidi.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com