Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA IMEFANYA MABORESHO MAKUBWA KATIKA MIFUMO YA TEHAMA KUONGEZA UFANISI UKUSANYAJI MAPATO YA SERIKALI


 Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba (katikati) akiwa pamoja na Mkurugenzi wa huduma kwa mlipa kodi (TRA) Bw. Richard Kayombo (kulia) wakiangalia jinsi ya kuskani kinywaji kwa njia ya mfumo wa kielektroniki (ETS) unaotolewa na kampuni ya SICPA ili kuhakiki stempu na kuhakikisha kinywaji ni salama kwa matumizi ya binadamu katika kampeni iitwayo “Hakiki Stempu, Linda Afya yako”.
Maafisa kutoka Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) wakionesha jinsi mfumo wa kuhakiki stempu kielektoniki (ETS) unavyofanya kazi, ETS ni mfumo unaotolewa na kampuni ya SICPA ili kuhakiki vinywaji kwa watumiaji na pia wafanyabiashara..

-ETS NI MFUMO SAHIHI KATIKA UKUSANYAJI WA KODI – TRA.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewekeza na kufanya maboresho makubwa katika mifumo ya TEHAMA yenye lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji, uwazi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali. Eneo mojawapo ambalo maboresho hayo yamefanyika ni katika stempu za Kodi za kieletroniki (ETS).

Mfumo huu wa stempu za kielektroniki umeunganishwa na mifumo ya TRA ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji/uagizwaji kwa maana ya idadi, ujazo pamoja na ubora na viwango vya bidhaa. TRA inapenda kuwahamasisha wananchi wanaotumia bidhaa hizo kushiriki kulinda afya zao kwa kutambua bidhaa halisi na halali kwa matumizi yao.

Vilevile kutokana na wakusanya kodi kukabiliwa na changamoto ya kujua viwango vya kweli vya kodi kwa uzalishaji uliopo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifikiria kutafuta njia nyingine ya kisasa na sahihi ili kukabiliana na changamoto hiyo. Ambapo kampuni ya SICPA ilipewa jukumu hilo na kuja na mfumo wa stempu wa kielektroniki (ETS).

Kufanikisha utendaji wakeTRA iliweka awamu kadhaa za utekelezaji wa mfumo, ambapo katika awamu ya kwanza ya mfumo, iliyozinduliwa Januari 15,2019 stempu za kielektroniki ziliwekwa kwa kampuni 19 zinazozalisha bidhaa za pombe, mvinyo na vinywaji vikali nchini.

Awamu ya pili ya stempu za kielektroniki iliyoanza Agosti 1,2019 ziliwekwa kwenye bidhaa kama vile maji yaliyotiwa ladha tofauti na kwenye vinywaji vingine visivyo vya kileo.

Katika mahojiano na Meneja Miradi wa TRA wa Mfumo wa ETS mapema mwaka jana, Innocent Minja alisema...Lengo kuu la kutafuta mfumo mpya wa ukusanyaji kodi na uzinduzi wa ETS miaka mitatu iliyopita ni kulinda mapato ya serikali na kusaidia watumiaji wa bidhaa za vimiminika kulinda afya zao.

"Tulikuwa na changamoto kubwa ya ukusanyaji wa kodi kutokana na watu kutokuwa wakweli na pia uwapo wa uzito katika ulipaji kodi kwa hiari.

“Awali tulilazimika kuweka maofisa wetu kuangalia uzalishaji na kuhakikisha watengenezaji wanatangaza viwango vya kweli vya uzalishaji. Hata hivyo, hali hiyo ilikuwa na changamoto nyingi na kuonekana kama vurugu tukahitaji suluhu mpya,” alisema Minja.

Minja alisema kutokana na baadhi ya wazalishaji kutokuwa wakweli kuhusu uzalishaji wao na hivyo kusababisha ushindani usio wa haki wa bidhaa zao sokoni na wale wanaosema kweli na kulipa kodi stahiki.

Pia Minja aliongeza kwamba mfumo wa ETS katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita umeimarisha ulipaji wa kodi na hivyo kuimarisha ushindani wa haki sokoni.

"Hii imesababisha kila mtengenezaji wa bidhaa iliyomo kwenye mfumo kulipa kodi kwa haki," alisema Minja.

Ufungaji wa ETS umehakikisha kuwa TRA inapata data za uzalishaji kwa wakati (muda halisi) kutoka kwa watengenezaji.

"Hii ni kwa sababu ya kodi ya ushuru kwa bidhaa maalumu hutozwa kwa kiwango cha uzalishaji hivyo kujua takwimu za uzalishaji ni muhimu."

Kama ilivyotarajiwa, kuanza kwa mfumo wa ETS uliambatana na uwapo wa vifungo vya usalama kwenye teknolojia husika na kurahisisha usimamizi wa kodi nchini.

“Mfumo ulileta uwazi kwenye kodi hasa kwenye kodi ya ushuru, Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi ya kampuni na hatimaye kupunguza manung’uniko ya walipa kodi,” alisema Minja.

Aliongeza kwa kusema ‘‘mchakato wa ufungaji ni endelevu haswa kutokana na viwanda kuendelea kuongeza viwango vya mitambo yao.’’

"Tayari tumeweka mfumo wa ETS kwa watengenezaji wote wanaostahiki wa bidhaa maalum. Takriban vifaa 135 vimefungwa kwenye viwanda vyenye mitambo inayojiendesha huku viwanda visivyojiendesha vikilazimika kuwasha mfumo huo kila wanapoanza uzalishaji,” alisema Minja.

Pamoja na kufanikisha uwekezaji wa mfumo mfumo wa ETS; mfumo huo umekuwa ni msaada mkubwa kwa wazalishaji na waingizaji wa bidhaa mbalimbali.

"Mfumo huu umeongeza uwazi, na kwa sasa, watengenezaji na waagizaji wa bidhaa zilizomo kwenye mfumo wanahakikishiwa usawa sokoni kwa kuwa kila mtu analipa ushuru wa kweli na sahihi wa bidhaa husika na kinyume na awali kabla ya mfumo."

Aliongeza kwamba ETS sio tu imerahisisha kadirio la makusanyo ya kodi, lakini pia mfumo umesaidia wazalishaji kutambua kiasi cha uzalishaji na muda ulitumika kuzalisha bidhaa husika. Pia imesaidia kujua changamoto zinazohusiana na mchakato wa uzalishaji na kutafuta suluhu za changamoto hizo. ETS ikitumika vizuri kwa usahihi malipo ya VAT pia yanakuwa sahihi na pia kurahisisha ukusanyaji na ulipaji wa kodi.

“Tunawaomba wazalishaji, waagizaji na wananchi kwa ujumla, kutumia kwa dhati mfumo huo na kuepuka matumizi ya stempu za kughushi,” anasema Minja na kuongeza kuwa TRA inafuatilia kwa makini ufanisi wa mfumo huo pote nchini.

Kuelekea Msimu wa Sikukuu TRA inatoa wito kwa watumiaji na wananchi kwa ujumla kupakua App ya Hakiki Stempu bure kwenye simu zao za kiganjani ambayo itawawezesha kutambua bidhaa inayofaa kwa matumizi ili kulinda afya zao pamoja na kuiwezesha serikali kukusanya kodi kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania. Vile vile inatoa wito kwa wazalishaji na waingizaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa kutumia mfumo wa ETS kwa uaminifu ili kulinda bidhaa zao sokoni dhidi ya bidhaa bandia pamoja na kusaidia makadirio halali ya kodi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com