Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza wa kifua kwa mgonjwa ili kuondoa uvimbe kwenye pafu kutumia tundu dogo moja uliowashirikisha watalaamu wazalendo ukiongozwa na Bingwa wa Upasuaji Kifua Duniani na mgunduzi wa upasuaji wa aina hiyo, Dkt. Diego Gonzalez Rivas kutoka nchini Hispania.
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji (MNH) Dkt. Rachel Mhaville amesema, upasuaji huu ni mwendelezo wa azma ya Serikali chini ya Wizara ya Afya wa kuhakikisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi zinatolewa nchini zenye kuleta unafuu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla ambao pia unaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutumia tundu moja dogo kupitia Hospitali ya umma katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ukilinganisha na matundu matatu yaliyozoeleka sehemu nyingine duniani.
Mkuu wa Idara ya Upasuaji, Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga Dkt. Ibrahim Mkoma amesema mgonjwa akifanyiwa upasuaji huo ambao siyo wa kufungua kifua anaweza asihitaji kukaa ICU kama wagonjwa wengine wa upasuaji wa kawaida na akaruhusiwa siku ya pili au ya tatu yake hivyo kuendelea na shughuli zake mapema zaidi.
Dkt. Mkoma amesema wagonjwa wapatao wanne wanategemewa kufanyiwa upasuaji wa aina hiyo na mara baada ya hapo watalaamuwazalendo wataendelea kutoa huduma hiyo kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali.