WANAFUNZI 9 WALIOMALIZA ELIMU MSINGI CHINI YA MTI WAMKOSHA MBUNGE WA KITETO



Na Mathias Canal, Kiteto-Manyara

Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mhe Edward Ole Lekaita amekoshwa na wanafunzi 9 ambao wamehitimu elimu ya msingi (Darasa la saba) leo tarehe 22 Septemba 2023 katika Shule ya Msingi Kititenebo ikiwa ni mahafali ya kwanza tangu kuanizshwa kwa shule hiyo.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo ya kwanza ya shule hiyo amewapongeza wanafunzi tisa wakiwemo wasichana wanne na wavulana watano kwa uvumilivu wao kwani walianza elimu ya msingi mwaka 2017 wakisomea chini ya mti lakini hatimaye wamehitimu elimu ya msingi.

Mbunge Ole Lekaita amesema kuwa huo ni uvumilivu wa hali ya juu kwani wasingekuwa wavumilivu wasingeweza kuhitimu elimu hiyo.

Amesema katika jamii ya kimasai mtoto kujitokeza na kusoma sio jambo jepesi hivyo wanapofanya hivyo ni muhimu kutoa pongezi kwa wazazi/walezi, walimu pamoja na wanafunzi wenyewe.

"Mimi ninawapongeza na kuwaombea sana kwani naamini mtafika mbali kutokana na juhudi mliyoionyesha ya kuanza elimu yenu chini ya mti na sasa mmehitimu mkiwa kwenye madarasa mazuri" Amekaririwa Mbunge Lekaita.

"Wanafunzi wenzenu wanaobaki wametoa wosia kwenu kwamba hamjamaliza shule bali mmehitimu darasa la saba, bado safari yenu ni ndefu ya sekondari, vyuo vikuu na mtakuwa wanasheria, wabunge, madaktari na wataalamu katika nchi yetu"

Amewataka wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii kwani serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira rafiki katika utoaji wa elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunza na ufundishaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post